Friday , 19 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Adhabu ya MAWIO yazidi kupingwa
Habari MchanganyikoTangulizi

Adhabu ya MAWIO yazidi kupingwa

Pili Mtambalike, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (wakwanza) na Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC)
Spread the love

ASASI mbili za kihabari na utetezi wa haki za binadamu zimesaini tamko la pamoja la kupinga uamuzi wa Serikali ya Tanzania wa kulifungia gazeti la MAWIO, kwa kipindi cha miezi 24 (miaka miwili), anaandika Hamisi Mguta.

Gazeti la MAWIO, linalochapishwa kila siku ya Alhamisi, limefungiwa kwa kipindi hicho kwa agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye tarehe 15 Juni mwaka huu alisaini barua ya kutangaza adhabu hiyo.

Sababu ambayo Waziri Dk. Mwakyembe ameitaja kama msingi wa kulifungia gazeti linalomilikiwa na kuchapishwa na Victoria Media Service Limited (VMSL), ni kutuhumu kuwa gazeti kupitia toleo lake Na. 196 la Juni 15-21, 2017, lilichapisha picha za marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na kwa lengo baya la kuwahusisha na kuwatuhumu kuhusika na mikataba ya madini.

Amekitaja kitendo hicho kuwa ni cha kuwadhalilisha viongozi hao wastaafu na hivyo kuhatarisha amani, utulivu na usalama wa nchi, kinyume cha Kifungu 59 cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12/2016.

Leo mchana, Wakurugenzi wa asasi za Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu Tanzania (THRDC) wamejitokeza hadharani na kulalamikia kitendo hicho cha serikali kufungia gazeti, wakisema hakikubaliki na kinatakiwa kubadilishwa.

Unaweza kutazama mwanzo mwisho kupitia video hapo chini…

Katika tamko hilo lililosomwa mbele ya waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya Baraza la Habari Tanzania, Mwenge jijini Dar es Salaam, wakurugenzi hao wamesema uamuzi huo unakiuka sheria za nchi zinazohusu haki ya kujieleza.

Bali hata kwa anga ya kimataifa, kwa kulifungia gazeti, serikali imekiuka Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) pamoja na Mkataba wa Afrika ambayo Tanzania imeridhia.

“Kwa kufungia gazeti, inasababisha wananchi wengi kunyimwa fursa ya haki yao ya kupata habari na kwa hivyo kupunguza kiwango cha uwazi katika uendeshaji wa serikali kwa sababu waandishi wa habari na vyombo vya habari ni kama wafuatiliaji wa namna serikali inavyoongoza watu,” tamko limesema.

“Kufungia gazeti la Mawio na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu dhidi ya vyombo vya habari na waandishi ni muendelezo wa nia ya serikali ya kuzuia ustawi wa uhuru wa watu kutoa maoni na kupata habari. Tayari Rais alishatamka hadharani kuwa uhuru wa habari una mipaka. Kwa hivyo uamuzi wa kufungia gazeti unaonesha ni utekelezaji wa mkakati wa kudhibiti uhuru wa watu kujieleza,” wamesema.

Tamko hilo lililosainiwa na Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga na Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu, Onesmo Olengurumwa, linasema waziri Mwakyembe ametumia vibaya mamlaka aliyopewa na sheria husika.

Hoja yao ni kwamba kifungu 59 cha Sheria ya Huduma za Habari kinampa uwezo waziri wa habari kuzuia au kuagiza kusitishwa kwa uchapishaji wa taarifa yoyote inayohatarisha usalama wa nchi na usalama wa jamii.

Hata hivyo, wanasema hawaamini wala hawaoni kwa vyovyote vile kuwa gazeti kwa kuchapisha picha za marais wastaafu limehatarisha usalama wa nchi na jamii.

Badala yake, wanaona uchapishaji wa picha hizo pamoja na makala ya mchangiaji inayohoji uadilifu wa viongozi hao, ni hatua ambayo ingetumiwa na Serikali, Bunge na wengineo kutafuta ufumbuzi wa namna nzuri ya kutumia raslimali za nchi.

Wametaka serikali ifute uamuzi wake kwa kuzingatia kwamba si wa kidemokrasia na unajenga picha mbaya kwa nchi kwamba serikali ya Tanzania inaendekeza ukiukaji wa uhuru wa watu kupata habari na kujieleza ambao unalindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Wakuu wa asasi hizo pia wameishauri serikali kurudisha sheria hiyo bungeni ifanyiwe marekebisho ili kuondoa vifungu vinavyozuia uhuru wa watu kupata habari na kujieleza. Uhuru huo unalindwa vema na Katiba ya nchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

error: Content is protected !!