CHAMA cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimesema kauli za kisiasa zinazoendelea kutolewa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusiana na mgogoro wa uongozi unaokikabili Chama cha Wananchi (CUF) zinaweza kuhatarisha usalama wa taifa na zinaingilia uhuru wa Mahakama, anaandika Hamisi Mguta.
Doyo Hassan, Katibu Mkuu wa ADC, amesema hayo leo katika mazungumzo yake na waandishi wa habari ofisini kwake Buguruni, Dar es Salaam. Mkutano huo ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka mitano ya kuzaliwa kwa chama hicho.
Bila ya kuzitaja kauli zenyewe lakini akimtaja mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea kama mtoa kauli mkuu, Doyo amesema “Chadema ina usajili wake na CUF wana usajili wao. Vyama hivi vinahusianaje? Wanajitokeza kwenda kusema wanakwenda kumuondoa Mwenyekiti wa chama kingine, je chama hicho kikimpiga Kubenea itakuaje?
“Kauli hizi zinazotoka CUF wakijipanga wakaenda kumshughulikia Kubenea au Kubenea akidundwa huko atasema hawa ni CUF kwa hiyo unaweza ukaona kauli zinazoendelea zinaweza kuhatarisha usalama wa taifa letu.”
Doyo amevitaka vyombo vya dola kudhibiti kauli hizo kwani CUF wapo mahakamani na kitendo cha kusema Chadema wanataka waende kumuondoa Mwenyekiti wa CUF kama taasisi nyingine maana yake wanaidharau mahakama.
“Tumeshuhudia migogoro mingi ya vyama vya siasa lakini hatujaona kingine kikiingilia mgogoro wa chama kingine,” amesema Doyo ambaye pamoja na wenzake kadhaa walianzisha ADC baada ya kutimuliwa CUF mnamo Desemba 2012.
CUF imeingia katika mgogoro pale Profesa Ibrahim Lipumba aliyekuwa mwenyekiti lakini akajiuzulu kwa hiari yake tarehe 5 Agosti 2015, alipotangaza kutengua uamuzi wake huo na kutaka kurudi ofisini.
Chama kilipofanya mkutano mkuu maalum tarehe 21 Agosti 2016, ili kuchagua mwanachama wa kujaza nafasi hiyo na nyinginezo zilizokuwa wazi, Prof. Lipumba aliingilia mkutano huo kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza na kusababisha tafrani iliyolazimu mkutano kuvunjika.
Katika hatua nyingine, Doyo ameitaka Serikali kuacha kuvizuia vyama vya siasa nchini kufanya shughuli za kisiasa, akishikilia kuwa kuvizuia si tu ni kuvikandamiza dhidi ya haki yao ya kikatiba, bali pia ni kujenga picha mbaya ya kwamba serikali inatawala kwa mkono wa chuma.
Pia Doyo ameibana serikali kuchukua hatua zifaazo kudhibiti mauaji mabaya ya kuvizia yanayofanywa wilayani Kibiti na kulaani kwa wanaoyaendeleza.
Maadhimisho ya kuzaliwa kwa ADC yatafanyika tarehe 22 mwezi ujao kwa viongozi kufanya ziara kwenye asasi za kiraia, kuwatembelea wagonjwa, wafungwa, vyuo vikuu na kutembea asasi ya Mwalimu Nyerere Foundation sehemuj ya Kigoda cha Mwalimu Nyerere.
Leave a comment