May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ADC wampitisha Maimuna kumvaa Dk. Tulia nafasi ya Uspika

Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid Mohamed akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)

Spread the love

CHAMA Cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimempitisha Maimuna Said Kassim kuwa mgombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni wiki chache baada ya aliyekuwa Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai kujiuzulu. Anaripoti Mwanaharusi Abdallah – TUDARCo … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 22 Januari, 2022 katika Ofisi za chama hizo zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Taifa wa ADC, Hamad Rashid Mohamed amesema chama hicho kimempitisha Maimuna baada ya kamati tendaji ya chama kujiridhisha kuwa ana uwezo na elimu ya kutosha.

Amesema mgombea huyo pia ana weledi wa kutosha hivyo anaweza kuwaongoza wabunge kama kiongozi mkuu wa mhimili huo.

Ameongeza wabunge wa chama tawala – CCM wamekuwa na hulka ya kumchagua Spika anayetokana na chama chao bila kujali uwezo wake hali ambayo inachangia kuleta migongano ya kimihimili ndani ya nchi.

Mgombea wa nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Maimuna Said Kassim akizungumzia na waandishi wa habari kuhusu uteuzi wake

“Hatuna mashaka hata kidogo na uwezo wa Maimuna Said kwani hata katika uchaguzi mkuu uliopita aligombea ubunge katika jimbo la Kilindi na alipata kura 18,000, hivyo ana uwezo wakusimamia na kuliongoza Bung. Ninawaomba wabunge wote kumpa kura za ndio” amesema Mwenyekiti huyo.

Aidha, amesema ADC hakipeleki mgombea kwa kutafuta wasifu kama inavyozungumzwa lakini chama hicho kinaamini katika misingi ya uongozi unaopatikana kwa kufuata taratibu za kushiriki kwa wanachama wake kugombea kwani ndio moja ya sifa ya chama hicho.

Ameongeza kuwa chama hicho moja ya kazi yake ni kupika viongozi bora wenye weledi na matunda yake tayari wana kiongozi ndani ya serikali ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga na sasa wanakwenda kutoa kiongozi mwingine wa mhimili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, amempongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya hasa kuwaunganisha watanzania na maendeleo ya nchi ambayo yanaonekana katika kipindi hiki kifupi alichohudumu hivyo wao kama ADC wataendelea kumuunga mkono.

Kwa upande wake Maimuma amesema anakishukuru Chama chake kwa kumuamini, na kumuona anafaa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nilijitathmini nikaona nina uwezo, elimu ya kutosha kwa sababu nimesomea masuala ya kibunge hivyo nina hakika kama wabunge watanichagua nitafanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa” amesema Maimuna.

Hata hivyo, amesema atalifanya Bunge kuwa la kisasa kwani katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na migongano ya mihili.

error: Content is protected !!