Monday , 4 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa ACT yazidi kuikaba serikali
Habari za SiasaTangulizi

ACT yazidi kuikaba serikali

Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa Tanzania, akikagua chakula cha hifadhi wakati wa utawala wake
Spread the love

CHAMA Cha ACT-Wazalendo sasa kinataka serikali imwelekeze Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum kwenye utoaji wa vibali vya kuuza chakula nje mwaka jana, anaandika Pendo Omary.

Uongozi wa chama hicho umekuja na rai hiyo katika kukazia hoja ya kiongozi wao mkuu, Zitto Kabwe ya kuweka rehani ubunge wake iwapo atathibitishiwa na serikali kwa kuona mwenyewe kuwepo kwa tani 1.5 milioni za chakula kwenye maghala ya akiba yanayosimamiwa na Wakala wa Chakula cha Akiba nchini (NFRA).

Leo Ado Shaibu, Katibu wa Kamati ya Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi wa ACT Wazalendo ametoa taarifa ya maandishi ikisema kuwa hoja ya chama inasimamia takwimu rasmi za serikali zilizotolewa katika njia mbalimbali mwaka jana.

Shaibu amesema serikali inaposema kwamba imeelekeza kuanza kusambazwa chakula kipatacho tani milioni 1.5 zilizopo kwenye maghala yake ya akiba, inaonesha kuna kitu hakisemwi kwa ukamilifu wake.

Amesema Zitto anaposhikilia hoja ya kuweka rehani ubunge wake anazingatia takwimu rasmi zilizotolewa na serikali kupitia vyombo vyake. Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, kufikia mwezi Oktoba mwaka jana kulikuwa na akiba ya chakula tani 90,476 kwenye maghala yake.

Maeneo yote yanayotajwa kuwa na tishio la njaa,ukweli ni kwamba chakula pekee ambacho serikali inakimiliki na ina uwezo wa kukisambaza ni kile kilicho NFRA, ambacho mpaka mwezi Oktoba kulikuwa ni tani 90,476 tu.

Akinukuu taarifa ya Wizara ya Fedha na Mipango ya mwezi Juni mwaka jana kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa, Shaibu amesema uzalishaji wa mahindi kwa msimu uliopita, ulipungua kwa asilimia 12.3 wakati uzalishaji wa ngano na mtama/uwele ulipungua kwa asilimia 57 na asilimia 19 kwa mfuatano huo.

“Serikali inatoa wapi hizo tani milioni 1.5? Je, inaahidi kusambaza chakula hewa?,” amehoji Shaibu katika hoja ya ACT-Wazalendo inayolalia taarifa zinazohusu mavuno ya msimu uliopita.

Shaibu amesema mchele tu ndio uzalishaji wake uliongezeka kwa asilimia 15, ndiyo maana “Serikali ilitoa vibali vya kuuza mchele nje baada ya kuwa soko la ndani limejaa mchele kutoka Pakistan na kadhalika.”

Anasisitiza kwamba kwa kuongezea vibali vilivyotolewa na serikali vya kuuza mahindi (au unga wa mahindi) nje, “utaona kuwa kuna kila sababu ya kutaka ukaguzi maalumu wa mdhibiti kwenye mchakato wa utoaji wa vibali vya kuuza nafaka nje ya nchi.”

Amesema “Tunaiomba ofisi ya CAG ifanye ukaguzi maalumu kukagua vibali vya kuuzwa chakula nje mwaka jana ili kujua ukweli wa jambo hili. Likithibitika kuwa ni kweli ni wazi kuwa serikali itabidi iwajibike kwa kuweka mbele maslahi ya kibiashara badala ya maslahi ya maisha ya wananchi.”

Jana Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini alitangaza kuweka rehani ubunge wake iwapo kutakuwa na uthibitisho wa serikali kumiliki chakula cha akiba kipatacho tani 1.5 milioni. Tamko lake lilikuja baada ya Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu kutangaza kwamba serikali itaanza kusambaza chakula kwenye maeneo yenye uhaba huku akipinga taarifa kupitia vyombo vya habari kwamba kuna balaa la njaa nchini.

Waziri Mkuu Majaliwa aliyekuwa katika uzinduzi wa safari za ndege za ATCL kati ya Dodoma na Dar es Salaam, aliongeza shutuma kwa vyombo vya habari kutumika na baadhi ya wafanyabiashara kueneza taarifa alizosema si sahihi na zinatolewa ckwa maslahi ya wafanyabiashara wanaoingiza chakula nchini.

Msimamo huo unatokana na kauli ya Rais John Magufuli kutangaza kwamba hakuna uhaba wa chakula wala njaa popote nchini na kwamba hata wale wenye shida ya chakula kutokana na ukame katika msimu huu wasitarajie kupewa chakula bure na serikali.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwinyi aungana na Samia kuuaga mwili wa baba yake

Spread the loveRais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk....

Habari za SiasaTangulizi

Mtoto wa Mzee Mwinyi amwaga machozi

Spread the loveMtoto wa Hayati mzee Mwinyi, Abdullah Ali Hassan Mwinyi ameshindwa...

Habari za SiasaTangulizi

Mzee mwinyi alikuwa mwanademokrasia wa kweli

Spread the loveMtoto wa Hayati Ali Hassan Mwinyi, Abdullah Ali Hassan Mwinyi...

Habari za SiasaTangulizi

Samia: Mwinyi alikuwa maktaba inayotembea

Spread the loveRais Samia Suluhu hassan amesema Hayati rais mstaafu, Ali Hassan...

error: Content is protected !!