CHAMA cha ACT-Wazalendo kimewataka viongozi wa dini na viongozi wa serikali waliostaafu kukemea hujuma zinazojitokea katika uchaguzi Serikali za Mitaa kwani zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).
Mbarala Maharagande, Mratibu wa Mawasiliano wa Uchaguzi wa Serikali Mitaa ndani ya ACT-Wazalendo, amesema viongozi wa dini na wale wastaamu wamekuwa mstari wa mbele kuhimiza amani nchini lakini wamekuwa kimya kukemea vitendo vinavyoashiria kupotea kwa amani wanayoinadi kila siku.
“Viongozi wa dini na wastaafu mara nyingi wamekuwa wakisisitiza na kuhamasisha kulinda amani, lakini hawaonekani kuhimiza kutendwa kwa haki na kukemea viashiria vya kupotea kwa amani na utulivu,” amesema Maharagande.
Amedai kuwa endapo vitendo vinavyofanywa na wasimamizi wa uchaguzi visipokemewa vitaharibu uchaguzi.
Amesema kuwa kinachodaiwa kuwa ni dosari na Waziri wa Tamisemi, Suleman Jaffo siyo kweli, ukweli ni hujuma zinafanyika kwa vyama vya upinzani.
Amezitaja miongoni mwa hujuma wanazozidai ni Serikali kutofanya maandalizi yanayostahili juu ya uchaguzi huu na kufungwa ofisi za wasimamizi wa uchaguzi, kukosekana mihuri, vitisho na, wasimamizi kudai mambo yasiyoelezwa na kanuni na sheria (utambulisho toka Mkoani), jeshi la polisi kutochukua hatua sahihi kudhibiti uhalifu.
Amezitaka mamlaka zinazohusika kudhibiti matendo yanayofanywa na watendaji hao yatakayosababisha kupandikiza chuki, uhasama miongoni mwa jamii.
Leave a comment