October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Wazalendo yatoa sababu kushiriki chaguzi

Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo

Spread the love

 

BAADA ya chama cha siasa nchini Tanzania cha ACT-Wazalendo kuibuka washindi wa Jimbo la Konde-Pemba visiwani Zanzibar, chama hicho kimetosa sababu kuu tatu zilizowafanya wakajitosa kwenye uchaguzi huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

ACT-Wazalendo kimejitokeza kuzungumzia chaguzi hizo, baada ya kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Konde na kushindwa Jimbo la Ushetu, mkoani Shinyanga na kata kadhaa uliofanyika Jumamosi ya tarehe 9 Oktoba 2021.

Katika uchaguzi huo, Mohamed Said Issa aliibuka mshindi Jimbo Konde kwa kupata kura 2391 kati ya kura 3,338 zilizopigwa huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiibuka kidedea Jimbo la Ushetu kwa Emmanuel Cherehani kushinda kwa kupata kura 103,357 sawa na asilimia 96.6 ya kura zote zilizopigwa.

Leo Jumatatu, tarehe 11 Oktoba 2021, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amezungumza na waandishi wa habati makao makuu ya chama hicho, Makumbusho, Dar es Salaam ambapo amesema, wao wataendelea kushiriki chaguzi kwani ni majukwaa sahihi ya kujijenga na kupeleka ujumbe kwa wananchi.

“Sisi kila uchaguzi ni somo, tukimaliza uchaguzi mmoja tunafanya tathimini kisha tunasonga mbele lakini katika haya majukwaa ya kampeni za uchaguzi, tunayatumia kupigania demokrasia kama kudai katiba mpya, tume huru ya uchaguzi na utawala bora,” amesema Ado

Amesema, chaguzi ndogo kama za Konde, Ushetu, Pandani, Muhambwe, Buhigwe na katika kata 15 za mikoa mbalimbali zinawapa somo na kutumia majukwaa hayo kujijenga zaidi siku kwa siku.

Ado amebainisha sababu kuu tatu zilizowafanya kushiriki chaguzi hizo za marudio ni kukipa fursa chama kuyatetea majimbo na kata walizokuwa wakiziongoza iwapo mbunge au diwani wa ACT Wazalendo atafariki au kupoteza sifa za kuendelea kushikilia nafasi yake.

“Mathalani, kwenye majimbo ya Pandani na Konde, chama kilishiriki kwa ajili ya kutetea nafasi yake kwa sababu majimbo hayo yalikuwa yanaongozwa na ACT Wazalendo kabla ya chaguzi za marudio kuitishwa,” amesema

Pia, amesema sababu nyingine ni, kupambana kushinda majimbo na kata ambazo “hatuziongozi na/au kujenga mtandao madhubuti wa chama. Katika hizo chaguzi zote tumefanikiwa kuongeza wanachama na kupanua mtandao wa chama.”

Mohamed Said Issa, mgombea wa ACT Wazalendo aliyeshinda Ubunge jimbo la Konde

Tatu, Ado amesema “kupigania demokrasia kupitia majukwaa ya kampeni. Kupigania katiba mpya na tume huru za uchaguzi za Tanzania na Zanzibar.”

“Uzoefu katika chaguzi zilizopita za marudio unaonesha kuwa kuna maeneo machache ambayo mamlaka za usimamizi wa uchaguzi zimepiga hatua na kufanya maboresho machache hasa kwenye mawasiliano na wadau, kupungua kwa changamoto katika uteuzi, kampeni na uapishaji wa mawakala,” amesema

Ado amesema, licha ya maboresho hayo machache, bado zipo changamoto mbalimbali zinazozikabili chaguzi za marudio ambazo ni “Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupanga muda mdogo sana wa kampeni wa wiki mbili hadi tatu ambao kwenye majimbo makubwa hasa ya Bara hautoshi kupiga kampeni kwenye maeneo yote na kuratibu upatikanaji na uapishaji wa mawakala kwa wakati.”

error: Content is protected !!