Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko ACT-Wazalendo yataka mchakato marekebisho sheria za habari ushushwe kwa wananchi
Habari Mchanganyiko

ACT-Wazalendo yataka mchakato marekebisho sheria za habari ushushwe kwa wananchi

Waandishi wa habari
Spread the love

CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimeshauri wananchi wapewe fursa ya kushiriki katika mchakato wa marekebisho ya sheria zinazosimamia sekta ya habari, ili watoe mapendekezo yao juu ya namna ya kuondoa sheria zinazokandamiza haki yao ya kupata habari. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Wito huo umetolewa jana tarehe 25 Novemba, 2022 na Msemaji wa Sekta ya Habari, Mawasiliano na Uchukuzi wa ACT-Wazalendo, Mwalimu Philbert Macheyeki, akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu.

“Ingependeza kama maoni ya wananchi yachukuliwe pia sababu uhuru wa habari hauangalii waandishi wa habari peke yake, unawahusu pia wananchi wanaopata habari kupitia maoni mbalimbali yanayotolewa na vyombo vya habari. Lazima wananchi wapate nafasi ya kufahamu nini kinaendelea sababu picha inaonyesha hawajashirikishwa ipasavyo,” amesema Mwalimu Macheyeki.

Katika hatua nyingine, Mwalimu Macheyeki ameshauri mapendekezo na maoni yaliyotolewa na wadau kuhusu marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016, yazingatiwe wakati Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ikiyafanyia kazi kwa ajili ya kuandaa muswada wa marekebisho yake utakaopelekwa bungeni kwa ajili ya kupatikana sheria mpya.

“Serikali ihakikishe maoni ya wadau yanazingatiwa sababu hao ndiyo wenye tasnia na kwamba maoni yao yanakwenda kuondoa kero za muda mrefu, hivyo yazingatiwe kabla ya kupelekwa kwa AG na kuundiwa muswada rasmi kwa ajili ya kupelekwa bungeni kuwa sheria mpya.

Kwa sasa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, inafanya mchakato wa marekebisho ya sheria zinazosimamia tasnia ya habari, ambapo wadau wametoa mapendekezo yao juu ya namna ya kuzirekebisha.

Miongoni mwa sheria za habari ambazo wadau wametoa mapendekezo yao, Sheria ya Takwimu ya 2015 iliyofanyiwa marekebisho 2018, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya 2016, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya 2018.

Hivi karibuni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye, alisema Serikali imeshafanya mapitio ya mwisho kuhusu mapendekezo yaliyotolewa na wadau juu ya maboresho ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na kwamba hatua inayofuata ni kupelekwa kwa AG kwa ajili ya kutungwa muswada.

Katika mapendekezo hayo, wadau wanapendekeza vifungu vinavyominya uhuru wa vyombo vya habari viondolewe ikiwemo vinavyoelekeza utoaji leseni kila mwaka, vinavyotafsiri makosa ya habari kuwa jinai badala ya madai na vinavyoipa mamlaka Serikali kuratibu shughuli za vyombo vya habari, hususan utoaji maudhui na upatikanaji wa matangazo.

Wadau wa tasnia ya habari waliotoa mapendekezo hayo ni pamoja na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CORI) na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA-TANZANIA).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyabiashara, wawekezaji China waridhia kuwekeza bil. 800 katika sekta 5 nchini

Spread the loveUJUMBE wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Jimbo la Changzhou...

Habari Mchanganyiko

Bil. 4.42 kumaliza uhaba maji kata 2 Musoma Vijijini

Spread the loveWANANCHI wa kata za Busambara na Kiriba, Jimbo la Musoma...

error: Content is protected !!