July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Wazalendo yapendekeza hatua nne upatikanaji katiba mpya

Dorothy Semu, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT wazalendo Bara

Spread the love

 

CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimeshauri mchakato wa upatikanaji katiba mpya uanze mara moja, huku kikitoa mapendekezo ya hatua nne za kuchukua kuelekea suala hilo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mapendekezo hayo ya ACT-Wazalendo yamewasilishwa na ujumbe wa chama hicho ukiongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, Dorothy Semu, leo Jumatatu, tarehe 23 Mei 2022, jijini Dar es Salaam.

Katika Kikosi Kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kupokea maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu uboreshwaji wa demokrasia ya vyama vya siasa.

Chama hicho kimependekeza hatua ya kwanza iwe ni upitiwaji upya na marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni, ili zikidhi matakwa ya muda.

“Mabadiliko hayo yataweza kuamua mchakato wa kupata katiba mpya uendelezwe kuanzia hatua ipi na pia kutambua maeneo yaliyosababisha mkwamo katika mchakato wa 2011 hadi 2014 na kuyafanyia marekebisho ili kuepuka mkwamo mwingine ikiwemo muundo wa wajumbe wa Bunge la Katiba au kama kuna haja ya kuja na mfumo mwingine wa chombo kingine cha kupitisha katiba mpya,” imesema taarifa ya ACT-Wazalendo.

Hatua ya pili iliyopendekezwa na ACT-Wazalendo, ni upatikanaji wa muafaka wa kitaifa kuhusiana na maeneo makubwa na muhimu yanayogusa mfumo wa kikatiba wa nchi ambayo yamekuwa chanzo na sababu ya mivutano katika maudhui ya katiba.

“Maeneo hayo ni pamoja na muungano na muundo wake, madaraka ya rais, mgawanyo wa madaraka kati ya Bunge, Mahakama na Serikali na mfumo wa uchaguzi na uendeshaji wake.
“Tunapendekeza utaratibu ule ule wa kuwa na mkutano wa majadiliano ya kitaifa utakaojumuisha Serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia, kidini, wasomi wabobezi sheria hasa katika maeneo ya katiba,” imesema taarifa ya ACT-Wazalendo.

Kwa mujibu wa taarifa ya ACT-Wazalendo, hatua ya tatu ni uundwaji wa timu ya watalaamu wabobezi kutoka ndani na nje ya Tanzania ambao watayaweka yaliyokubaliwa kwenye muafaka wa kitaifa kupitia mkutano wa majadiliano ya kitaifa.

Hatua ya mwisho iliyopendekezwa na ACT-Wazalendo, katiba mpya itakayopendekezwa kufikishwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

“Ambapo iwapo kama itaungwa mkono na wananchi walio wengi wa upande wa Tanganyika na wananchi walio wengi wa Zanzibar, basi itakuwa imeridhiwa na kuidhinishwa rasmi,” imesema taarifa ya ACT-Wazalendo kuhusu mapendekezo hayo.

Pia, chama hicho kimeshauri kama mchakato huo hautakimilika hadi Agosti 2024, usimamishwe kwa ajili ya kupisha chaguzi zijazo na kwamba baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 kukamilika, uendelee.

error: Content is protected !!