CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimeishauri Serikali ya Morocco iitishe kura ya maoni ili wananchi wa Sahara Magharibi, waamue kama wanakubali kuwa Taifa huru au waendelee kutawaliwa na serikali hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Wito huo umetolewa leo Jumanne, tarehe 17 Mei 2022 na Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, akizungumza katika maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Ado amesema, endapo Serikali ya Morocco itaacha kuitawala nchi ya Sahara Magharibi, kinyume na sheria za kimataifa na haki ya nchi kujitawala na kujiamulia mambo yake, wataenzi msimamo wa Mwalimu Nyerere wa kupinga nchi za Afrika kuendelea kutawaliwa.
“Ninafurahi kuyasema haya mbele ya Balozi wa Sahara Magharibi Ndugu Mahyub Sidina na Maafisa Waandamizi wa Ubalozi wa Morocco ambao mmehudhuria maadhimisho haya. Tanzania, kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, haiwezi kusemwa kuwa huru kama kuna Nchi yoyote ndani ya Afrika inaendelea kutawaliwa”-amesema Ado na kuongeza:
“Kitendo cha Morroco kuendelea kuikalia Sahara Magharibi kimabavu tangu 1975 hakikubaliki. Tunatoa wito wa kufanyika kura ya maoni ya Wananchi wa Sahara Magharibi, kuamua hatma yao kama ilivyoazimiwa na Umoja wa Mataifa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kura ya Maoni ya Sahara Magharibi (MINURSO), ukaundwa 1991.”
Maadhimisho ya Miaka 100 ya Kuzaliwa kwa Mwalimu Nyerere yalihudhuriwa na Viongozi Mbalimbali wa Serikali, Mabalozi, Wanazuoni, Asasi za Kiraia na Viongozi wa Vyama vya Kisiasa.
Leave a comment