August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ACT Wazalendo yamuangukia Magufuli

Spread the love

CHAMA cha ACT Wazalendo, kimemuomba Rais John Magufuli kuunda timu ya wataalamu ili kuipitia upya Rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba na kuitisha Mkutano Mkuu wa Kikatiba ili kuijadili, anaandika Aisha Amran.

Wakati chama hicho kikitoa maombi hayo, inafahamika wazi kuwa msimamo wa Rais Magufuli juu ya suala hilo ni kuendeleza mchakato wa Katiba mpya pale ulipoishia kwa kuitisha kura ya maoni ya Katiba pendekezwa.

Maombi hayo ya ACT Wazalendo ni miongoni mwa maazimio matatu yaliyotolewa na chama hicho kufuatia mkutano wao wa siku moja unaojulikana kama  mkutano wa kidemokrasia.

Abdallah Khamis, Ofisa Habari wa chama hicho, “Chama kimeazimia kumshauri rais aridhie mchakato wa kuandika Katiba mpya uanze kwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Kura ya Maoni na Sheria ya Mchakato wa Katiba,” amesema.

Khamis amesema kuwa iwapo serikali itaamua kuendeleaa na mchakato wa kupigia kura ya maoni Katiba pendekezwa, chama hicho kitaipinga kwa kufanya kampeni ya kupiga kura ya Hapana.

Itakumbukwa kuwa Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Katiba na Sheria,  alinukuliwa akisema kuwa Katiba mpya si kipaumbele cha Rais  Magufuli kwa sasa.

“Rais alipohutubia Bunge alisema kuwa, kuna kiporo cha Katiba ameachiwa na atakimalizia. sasa mimi nashangaa hawa watu, tena wengine wana Shahada za Sheria, wanaongea nini? Hatua ya rasimu ya Warioba ilishapitwa na wakati na kwasasa tayari tunayo Katiba pendekezwa,” alisema Mwakyembe tarehe 24 Februari mwaka huu.

Katika hatua nyingine chama cha ACT Wazalendo, kimeshangazwa na kitendo cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar kupitisha Sheria ya Kutafuta Mafuta na Gesi, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano inayotambua kuwa mafuta na gesi kuwa ni suala ya muungano.

“Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia umeshauri chama kimwelekeze Mbunge wake (Zitto Kabwe), awasilishe Bungeni hoja binafsi ya kufanya mabadiliko ya kuondoa mafuta na gesi kuwa jambo la Muungano ili kuiwezesha Zanzibar kutafuta mafuta na gesi asilia bila vikwazo,” amesema Khamis.

error: Content is protected !!