CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimesema changamoto zinazoikabili Bandari ya Malindi, Zanzibar, haitokani na kuwa na gati moja, kama ilivyoelezwa na Rais wa visiwa hivyo, Dk. Hussein Mwinyi, bali inatokana na gharama kubwa za huduma wanazotozwa watumiaji wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 4 Machi 2023 na Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, Ismail Jussa, akizungumza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho, katika viwanja vya Tibirinzi, Pemba, visiwani Zanzibar.
Jussa amedai kuwa, mapato ya bandari za Zanzibar yamepungua kutokana na gharama kubwa za ushushaji mizigo ambapo gharama za ushushaji kontena lenye futi 40 ni dola 7,000 wakati bandari za nchi nyingine gharama zake zikiwa ni 2,000.
“Kwanza kasema changamoto katika bandari ya Zanzibar ni gati moja, sasa nataka kumuuliza kwani lini Zanzibar ilipata kuwa na gati mbili au tatu? Au tulikuwa na bandari kubwa ikawa ya kisasa, kwa nini zamani yalipokuwa makontena yakishuka hata pa kuyaweka hakuna, kulikuwa na gati moja na gharama haikufika ilipofika sasa,” amesema Jussa.
Naye Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema ni kazi rahisi kumuondoa madarakani Rais Mwinyi, kupitia Uchaguzi Mkuu wa 2025, kama kumsukuma mlevi.
“Hivi karibuni nilihojiwa na kituo kimoja cha televisheni na nikatoa maoni yangu hali ya kisiasa Zanzibar kuelekea 2025, nikawaeleza bila kupepesa macho kwamba hakuna mwaka rahisi na mwepesi kwa ACT-Wazalendo kushinda uchaguzi kama 2025,” amesema Shaibu na kuongeza:
“Hakuna mwaka rahisi kama kumsukuma mlevi, ushindi wetu utakuwa rahisi. Kumuondoa Rais Mwinyi itakuwa kazi rahisi sana, tuendelee kujipanga kuongoza. Tunapambana usiku na mchana kuhakikisha tunakwenda Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Mkuu tukiwa na tume huru ya uchaguzi.”

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Bara, Dorothy Semu, amewataka wanachama wa chama hicho visiwani Pemba, waendelee kusimama imara katika kuipigania demokrasia ya kweli.
“Sote tunafahamu kwamba, pamoja na changamoto lukuki, madhila makubwa na misukosuko mingi tuliyopitia kutafuta demokrasia ya kweli. Watu wa Pemba mmeendelea kusimama imara na kuonyesha hamyumbi mpaka tutakapopata demokrasia ya kweli katika nchi yetu,” amesema Semu.
Leave a comment