Wednesday , 29 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa ACT-Wazalendo yajipanga kujibu mapigo kwa Rais Dk. Mwinyi
Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yajipanga kujibu mapigo kwa Rais Dk. Mwinyi

Kaimu Naibu Katibu Mkuu ACT-Wazalendo-Zanzibar, Salim Bimani (Picha na Mintanga Hunda)
Spread the love

 

CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimeahidi kumjibu hadharani Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kufuatia kauli yake aliyotoa kuhusu sakata la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, iliyodai kwamba chama hicho kina maslahi kwenye suala hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Ahadi hiyo imetolewa leo Jumatano, tarehe 1 Machi 2023 na Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Salim Biman, alipoulizwa na mtandao huu kuhusu ufafanuzi wa kauli hiyo iliyotolewa na Rais Mwinyi, jana tarehe 28 Februari mwaka huu.

Bimani amesema kuwa, ACT-Wazalendo iliibua sakata hilo hadharani mbele ya umma kupitia mkutano wake wa hadhara uliofanyika Nungwi, visiwani Zanzibar, tarehe 24 Februari 2023 na kwamba kitamjibu Rais Mwinyi hadharani kupitia mkutano wake wa hadhara unaotarajiwa kufanyika Tibirizi, tarehe 4 Machi mwaka huu.

“Rais Mwinyi tumemsikia, maelezo yake yote ya jana tumeyasikia lakini kwa sasa hatusemi chochote. Sababu suala hilo tulilisema hadharani na tutamjibu hadharani, sisi tutakutana Tibirizi tarehe 4 Machi 2023,” amesema Bimani.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Zanzibar, Rais Mwinyi alitumia jukwaa hilo kujibu baadhi ya masuala yaliyoibuliwa na ACT-Wazalendo, katika mkutano wake wa hadhara wa Nungwi uliofanyika Jumapili iliyopita.

Ni baada ya waandishi wa habari kumtaka atoe ufafanuzi kuhusu masuala hayo ikiwemo madai ya upendeleo katika utoaji zabuni za kuhudumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, kufuatia Wakala wa Taifa wa Safari za Ndege Dubai (Dnata), kupewa haki pekee ya kutumia kituo cha tatu (Terminal three), kinachohudumia ndege za kimataifa.

Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, Rais Mwinyi alikanusha madai hayo akisema kwamba Serikali imeamua kuipa zabuni kampuni hiyo baada ya kampuni za awali kushindwa kuwasilisha mapato serikalini.

Rais Mwinyi alisema kuwa, kwa zaidi ya miaka 25 kampuni hizo zilipokuwa zinafanya kazi Serikali ilikuwa haipati chochote kiasi kwamba ilikuwa inatoa fedha hazina kwa ajili ya kulipa watumishi wa uwanja huo.

Kiongozi huyo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, alisema tangu kampuni ya Dnata ipewe zabuni katika uwanja huo, mapato yaliongezeka hadi kufikia Sh. 8.8 bilioni kwa robo mwaka iliyomalizikia Desemba 2022.

“Awamu ya nane tumeingia airport ilikuwa inapata hasara, Serikali ilikuwa inatoa fedha kutoka hazina kupeleka airport kulipa mshahara. Lakini mwezi uliopita makusanyo ya parking yalikuwa Sh. 139 milioni wakati zamani Serikali ikuwa inapewa Sh. 2 milioni, mbona hayo hamsemi?” alihoji Rais Mwinyi.

Dk. HUssein Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Rais Mwinyi alisema “uungwana unataka utangaze maslahi binafsi, kama una maslahi binafsi useme. Hao wanaotaka wana maslahi gani? Upo uhusiano kati ya hizo kampuni na viongozi, mbona hawasemi? Hapa hawaitetei Serikali na nchi wanatetea maslahi binafsi, hizi kampuni wanazotetea haziingizi chochote.”

Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi alihoji kwa nini chama hicho kimeishia kutoa changamoto zinazoikabili Bandari ya Malindi, badala ya kuonyesha jitihada zinazofanywa na Serikali kuzitatua.

“Changamoto za bandari ya Malindi zinasababishwa na jambo moja kuu, nalo kuwa na gati moja wakati meli ziko 10 hivyo lazima zitasubiri, na mpango wa Serikali kujenga Mangapwani kwa lengo hilo. Kuendelea kulaumu kitu ambacho kimekuwepo miaka yote sidhani kama sahihi. Mipango yote ya Serikali kuwa na bandari nyingi wanaijua waliozungumza lakini hawakutaka kusema,” alisema Rais Mwinyi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!