KAMATI Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo imeitaka Seriakali kutoa ratiba ya mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya na ule wa kupata Tume Huru ya Uchaguzi kama ilivyoamuliwa na Kikosi Kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Chama hicho kimetaka kuwekwa wazi hasa kwa hatua muhimu kama vile kupitiwa upya kwa sheria ya Mabadiliko ya Katiba, na Sheria ya kura ya maoni; kuitishwa kwa Mkutano wa Majadiliano ya Kitaifa kuhusu Katiba; kuundwa kwa Kamati ya Wataalam wa kuandaa rasimu ya Katiba na kupigwa kwa kura ya maoni.
Takwa hilo ni miongoni mwa maazimio ya Kamati Kuu ya Chama hicho iliyoketi jana jijini Dar es Salaam na kutolewa leo mbele ya waandishi wa ahabri na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu.
“Kamati Kuu ya ACT Wazalendo inazitaka Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar kuweka wazi kalenda ya utekelezaji wa mapendekezo ya Ripoti za Vikosi Kazi vya Demokrasia,” amesema Shaibu.
“Aidha, Kamati Kuu inazitaka Serikali za Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, ziweke bayana kalenda na mchakato wa uundwaji wa Tume Huru ya Uchaguzi. Kamati Kuu ya ACT Wazalendo inataka maelezo ya kina kuhusu uundwaji wa Kamati ya Uteuzi ya Wajumbe wa Tume za Uchaguzi NEC na ZEC (Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Mkurugenzi na Wajumbe) na upatikanaji wa Wajumbe hao,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine Kamati Kuu ya chama hicho imesema baada ya kupokea Taarifa ya Hali ya Kiuchumi nchini “ambayo inaonesha hali ngumu ya maisha kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu na kushamiri kwa migogoro ya ardhi,” imetoa maelekezo kwa Kamati ya Wasemaji wa Kisekta kufanya uchambuzi wa kina wa hali ya nchi kiuchumi na hatua za kuchukua kuukwamua.
Leave a comment