July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Wazalendo yabisha hodi kwa CAG

Spread the love
CHAMA Cha ACT-Wazalendo jana kimewasilisha rasmi hesabu zake katika Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya sheria kwa chama hicho, anaandika Aisha Amran.
Hatua hiyo inafuatia agizo walilopewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuvitaka vyama ambavyo havikuwasilisha hesabu zake kwa CAG kutekeleza jambo hilo ndani ya miezi mitatu kuanzia Aprili 27 mwaka huu.
Katika barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya Aprili 27 kwenda kwa Chama cha ACT-Wazalendo, Msajili aliwaeleza kwamba, baada ya muda wa miezi mitatu kupita kama chama hicho kitashindwa kuwasilisha hesabu zake katika Ofisi ya CAG, watapaswa kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua za kisheria.
Akizungumza na MwanaHalisionline mara baada ya kuwasilisha mahesabu yao kwa CAG, Abdallah Khamis, Ofisa Habari wa ACT-Wazalendo amesema, tarehe 20 Oktoba mwaka jana waliwasilisha hesabu zao katika Ofisi ya Msajili na baadaye msajili aliwaelekeza wawasilishe katika Ofisi ya CAG.
“Baada ya kuwasilisha hesabu zetu katika Ofisi ya Msajili, tulipata barua iliyotuelekeza tupeleke hesabu zetu kwa CAG na wakati huo ndio tulikuwa katika mchakato wa uchaguzi wa marudio katika baadhi ya majimbo hali iliyotufanya tughafilike,”amesema Khamis.
Amesema kuwa, mfumo wa chama hicho ni wa uwazi hali inayowafanya watoe mahesabu yao ya ndani na kuweka hadharani kila baada ya miezi mitatu.
Katika taarifa ya CAG iliyosomwa bungeni hivi karibuni ni chama kimoja pekee kilichotajwa kupeleka hesabu zake katika ofisi ya CAG.
Wakati huo huo Khamis amesema, maadhimisho ya kitaifa ya kutimiza miaka miwili kwa chama hicho tokea kipate usajili wa kudumu yatafanyika katika Mkoa wa Pwani, Wilaya ya Mkuranga Mei 5.
Amesema, katika kuelekea siku hiyo ya maadhimisho, vingozi na wanachama wa ACT Wazalendo katika sehemu mbalimbali nchini wameanza kufanya kazi za kijamii ikiwa ni pamoja na kujitolea damu, kufanya usafi katika maeneo ya umma pamoja na kuwatembelea yatima na wazee walio katika makambi ya wasiojiweza.
error: Content is protected !!