September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Wazalendo watoa masharti 4 kushiriki uchaguzi 

Spread the love

CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimetoa masharti manne kwa serikali, ili kishiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Masharti hayo yametolewa leo tarehe 11 Novemba 2019, jijini Dar es Salaam na Joran Bashange, Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni na Uchaguzi ya chama hicho.

Amesema, sharti la kwanza ni uchaguzi huo kufutwa na mchakato wake kurejewa upya, ambapo la pili ni kanuni za uchaguzi huo zitungwe upya sambamba na kuahirisha tarehe ya uchaguzi huo.

“Mchakato wote ufutwe na uanze upya, tukitaka kutenda haki kweli. Waahirishe tarehe, hakuna uchaguzi. Zitungwe kanuni za kuondoa watu, ziwekwe mpya na zifanyike kwa maridhiano na wadau wote hususan wanasiasa,” amesema Bashange.

Sharti la tatu ni uundwaji wa Kamati Huru ya Uchaguzi na isisimamiwe na Wizara ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambapo shatri la nne ni Seleman Jafo, Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuitisha kikao cha maridhiano na vyama vya siasa, juu ya namna ya kushiriki uchaguzi huo.

“Iundwe kamati huru ya uchaguzi na isisimamiwe na Tamisemi ambayo haina Uhuru wa kusimamia uchaguzi huu. Baada ya kupewa maelekezo ya Rais John Magufuli. Tuwe na chombo huru kamati huru,” amesema Bashange na kuongeza;

“Aitishe kikao cha pamoja na vyama, ili kuweka makubaliano na maridhiano ya namna gani uchaguzi huu ufanyike kwa haki.”

Wakati huo huo, Bashange ametoa wito kwa vyama vya siasa vya upinzani kutoa tamko la pamoja la kudai Tume Huru ya Uchaguzi.

“Tunatoa wito kwa vyama vya siasa, kukaa kikao cha pamoja ili kutoa tamko la pamoja kudai Tume Huru ya Uchaguzi. Pasipo hivyo, ghiliba na bao la mkono litaendelea,” amesema Bashange.

Amesema, Jafo ameweka mpira kwapani na kuondoka nao, na kwamba wao hawako tayari kumkimbiza.

“Tunasisitiza msimamo wetu na kuwataka wanachama nchi nzima, kwamba waendelee kuandika barua za kujiondoa mpaka pale mapendekezo yetu yatakapofanyiwa kazi. Maazimio ya vikao vyetu hayawezi kupanguliwa na matamko ya Jafo,” ameeleza Bashange.

Bashange ameeleza, bila mapendekezo yao kufanyiwa kazi, tabia ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupoka haki ya wananchi kuchagua viongozi wao, haitakoma.

“Hulka hii mbaya ya CCM ya kuendelea kupoka haki ya wananchi ya kuchagua viongozi wao, na kuwapanga viongozi wanavyotaka wenyewe, wakome.

“Tunaitaka serikali ikomeshe utaratibu huu. Sisi hatuwezi kuvumilia, tamko letu liko palepale. CCM imevuka mstari wa demokraisa, tusilaumiane,” amesema Bashange.

error: Content is protected !!