Thursday , 30 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa ACT-Wazalendo wataka Askofu Mwamakula kuachiwa huru, asidhihakiwe
Habari za SiasaTangulizi

ACT-Wazalendo wataka Askofu Mwamakula kuachiwa huru, asidhihakiwe

Emmaus Mwamakula
Spread the love

 

CHAMA cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania, kimelaani hatua ya jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, kumkamata na kumshikilia Askofu Dk. Emmaus Mwamakula, kwa madai ya kuhamasisha maandamano. Anaripoti Hamis Mguta…(endelea).

Taarifa ya chama hicho iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Idara ya habari na uenezi, Janeth Rite, imelitaka jeshi hilo kumuachia mara moja Askofu Dk. Mwamakula kwa kuwa hakuna sheria yoyote aliyoivunja.

“Askofu Dk. Mwamakula amejitolea kuhamasisha kwa njia za amani, uwepo wa mabadiliko ya katiba ya nchi itakayotoa fursa ya kuundwa kwa Tume huru ya uchaguzi. Kwa msingi huo, mpaka hapo, hakuna kosa lolote ambalo Askofu amelifanya,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kiongozi huyo wa kiroho na Kijamii, amekamatwa katika kipindi ambacho amekuwa akihamasisha matembezi ya hiari yenye lengo la kushinikiza kutekelezwa kwa matakwa yake hayo mawili – katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.

“Matembezi ya hiari, ni haki yake ya kikatiba kama raia wa Jamhuri ya Muungano. Kama kweli kuna makosa katika hili, jeshi la Polisi mbona halijaeleza sheria ipi iliyovunjwa kwa kuandaa matembezi ya hiari,” inahoji taarifa hiyo.

ACT- Wazalendo wanasema, “kama jeshi la Polisi, linadai matembezi ya hiari ni maandamano yasiyokuwa na kibali, walijuaje kama Askofu Mwamakula asingetoa taarifa rasmi ya kufanyika kwa matembezi yake?

“Kuhamasisha matembezi ya hiari kunahitaji kibali cha Polisi? Mbona madai haya ya Askofu Mwamakula yamekuwapo muda mrefu na mbona hayaleta taharuki?”

Kwa mujibu wa chama hicho, Ibara ya 20(1) ya Katiba ya Jamhuri, inatoa haki kwa kila raia kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, jeshi la polisi, linamshikilia Askofu Dk. Mwamakula kwa tuhuma za uchochezi.

Mambosasa amesema, kuna ‘clip’ inayozunguuka kwenye mitandao ya kijamii ambayo imetumwa na Dk. Mwamakula, inayohamamisha kufanyika matembezi ya hiari na ambayo ni kinyume na sheria.

Askofu Mwamakula anatuhumiwa kuhamasisha maandamano ambayo mwenyewe ameita, “ya amani na yanayolenga kushinikiza serikali kuruhusu uwapo wa Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.”

Chama hicho ambacho ni sehemu ya serikali katika sehemu moja ya Jamhuri – Visiwani Zanzibar – kinasema, ni matarajio yake kuwa Askofu Mwamakula, ataachiwa huru bila masharti.”

ACT- Wazalendo kinasema, kuendelea kumshikilia Askofu Mwamakula kwa kutekeleza haki yake kikatiba, ni kosa kisheria.

Kinasema, “Jeshi la polisi liache kufanya kazi za kisiasa zinazopora uhuru na haki zilizotolewa na katiba,” na kuongeza, “hata utaratibu uliotumika kumkamata Askofu Mwamakula, ni kinyume cha sheria.”

Katika hatua nyingine, chama hicho kimelaani kitendo cha Mambosasa “kumdhihaki” Askofu Mwamakula na kusema, “Jeshi la polisi halipaswi kuingilia uhuru wa kuabudu na kudhihaki hadhi ya kiongozi wa kiroho (Askofu).”

Katika taarifa yake kwa umma, Mambosasa alisema, jeshi lake linamshikilia mtu anayejiita, “Askofu wa Kanisa la Moravian Uamsho,” kwa tuhuma za kumahamasisha wananchi waingie barabarani kwa ajili ya madai ya tume huru ya uchaguzi na katiba mpya.

Alisema, hawakutegemea Askofu kuvunja sheria, lakini wali
poona “anashurutisha vurugu na katika kufanya vurugu kutakuwa vitendo mbalimbali vya uvunjifu wa amani, tulifungua jalada la uchunguzi.”

Kwa mujibu wa Mambosasa, jeshi lake halikutegemea kumuona Askofu anakimbilia kuvunja sheria. Alisema, “tunategemea Askofu anapokataza waumini wake wasitende dhambi, anaungana na serikali kukataza watu kufanya matendo ya kihalifu. Sasa kitendo chake cha kufanya kinyume, kimepelekea yeye kukamatwa na anaendelea kuhojiwa.”

SACP Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Jeshi la Polsii Kanda Maalumu ya Dar es Salaam

Alisema, “lakini nawaombe Watanzania wengine, ambao walisoma ile clip waipuuze, kwa sababu yeyote ambaye atajaribu kuungana naye kwa sababu zozote zile, ajue tutamkamata kama tulivyomkamata huyu anayehamasisha.

“Atahojiwa na mwisho atachukuliwa hatua kali za kisheria ili kuendelea kulinda nidhamu ya kutotaka kuvunja shera, lakini kuleta taharuki ndani ya jiji letu la Dar es Salaam.”

Hata hivyo, ACT – Wazalendo kinahoji, “ili mtu atambulike na jeshi la polisi kuwa ni Sheikh au Askofu, huwa kinatumia ithibati ipi? Jeshi la polisi linapata wapi mamlaka ya kuhoji juu ya cheo cha kidini cha mtu kwa mujibu wa imani yake?”

Kinaongeza, “Ibara ya 19 (1),(2) imeeleza wazi kuhusu uhuru wa mtu kuamini dini aitakayo. Kwamba, kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake.”

“Bila ya kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari ya mtu ya binafsi, na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.”

Kinasema, kinaunga mkono matembezi ya hiari yaliyoitishwa na Askofu Mwamakula. Kinaunga mkono madai ya uwepo wa tume huru ya uchaguzi na katiba mpya kwa kuwa yaliyotokea katika uchaguzi mkuu uliyopita, yametoa fundisho tosha.

“Katiba mpya ni ajenda endelevu ya wapenda haki na demokrasia isiyoweza kuzimwa kwa vitisho na mamlaka yeyote ile. ACT Wazalendo – kinataka Polisi kumuachia Askofu Mwamakula na kuacha ukandamizaji wa haki za kikatiba,” kimeeleza.

Askofu Mwamakula amekuwa akieleza umuhimu wa kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi itakayoheshimu misingi ya haki, demokrasia, pamoja na katiba mpya, tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa rais mwaka jana.

Katika uchaguzi huo, ambao mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli alitangazwa mshindi, Askofu Mwamakula alikuwa mmoja wa wapiga debe wakubwa wa aliyekuwa mgombea wa upinzani, Tundu Antipas Lissu.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa 28 Oktoba 2020, Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula, amejizoelea umaarufu mkubwa nchini, kutokana na ukosoaji wake dhidi ya serikali na msimamo wake wa kuwapo katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.

Anajitambulisha, pamoja na mambo mengine, kama mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani (World Fellowship of Moravian Revival Churches).

Amekuwa akitoa maandishi mbalimbali kupinga anachoita, “vitendo viovu” vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa umma, ikiwamo uvunjifu wa haki za kiraia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!