October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Wazalendo wapinga kinga ya Rais, Jaji Mkuu, Spika

Rais John Magufuli akiteta jambo na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma

Spread the love

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeleeza kuwa nia ya serikali ya kupitisha Muswada wa sheria mbalimbali Na.3 ya mwaka 2020 inalenga  kufunga milango ya kudai haki za binaadamu, utawala wa sheria na uwajibikaji, Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam …(endelea).

Muswada wa sheria hiyo unawapa kinga Rais, Spika wa Bunge, Makamo wa Rais na Jaji Mkuu ya kutoshtakiwa mahakamani.

Akizungumza na Waandishi wa Habari  leo tarehe 7 Juni 2020, Katibu Mkuu wa Chama hicho Ado Shaibu amesema kama muswada huo ukipitishwa bungeni wananchi watashindwa kwenda mahakamani kuiwajibisha serikali inapovunja Sheria au Katiba.

“Muswada  huu kama ukipitishwa na kuwa Sheria, utaturudisha nyuma sana kwenye mapambano ya kupigania uwajibikaji, utawala wa sheria na haki za binadamu.”amesema Ado.

Amesema kutokana na wingi wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bungeni  ambacho kipo madarakani muswada huo utapitishwa kwa kuwa una maslahi nao.

Ado amedai kuwa muswada huo ni miongoni mwa sababu za wananchi kupata hamasa za kukiondoa chama cha CCM kutokana na kujiwekea kinga ya kupinga kuwajibishwa.

Katika Muswada huo kuna marekebisho ya Kifungu namba 4 cha BRADEA kinarekebishwa na kusomeka kwamba, maombi ya kufungua kesi Mahakama Kuu hayatakubaliwa endapo hayajaambatanishwa na kiapo cha mlalamikaji kuelezea jinsi alivyoathiriwa na uvunjifu wa haki na wajibu katika ibara ya 12 hadi 29 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977.

Pia, Kifungu namba 7(4), ikiwa malalamiko ya uvunjifu wa haki unaelekezwa kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania au, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika wa Bunge, au Jaji Mkuu wa Tanzania, malalamiko hayo yatafungliwa dhidi ya mwanasheria mkuu wa serikali ikiwa na maana hakutakuwa na uwezekano wa kufungua kesi dhidi ya viongozi hao.

“Tumekuwa mstari wa mbele kuiwajibisha Serikali Mahakamani. Rais alipomwondosha CAG Prof. Assad kinyume na Katiba, Kiongozi wa Chama Ndugu Zitto Kabwe alimpeleka Mahakamani. Pia, Rais alipomteua Mwanasheria Mkuu wa Serikali asiye na vigezo vya kikatiba,  nilimpeleka mahakamani.” amesema.

Ado pamoja na kushindwa kwenye shauri lake alilomshtaki Rais juu ya kumteua Dk.  Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu amesema kuwa Mahakama ilitamka kuwa milango ya kumshtaki Rais Ipo wazi.

Hata hivyo katika Muswada huo uliopangwa kujadiliwa kwenye mkutano wa 19 wa Bunge (Mkutano wa Bajeti) ambao ulianza tarehe 05 Mei na utamalizika Juni 19 mwaka 2020 kuna marekebisho ya sheria ya uongozi wa Mahakama namba nne ya 2011, ambayo kifungu namba 64 (a) cha sheria hiyo kimerekebishwa na kuandikwa kuwa mfanyakazi yoyote wa mahakama hatoshtakiwa kwa jambo lolote atakalolifanya au kutolifanya kwa nia njema atakapokuwa anatekeleza majukumu yake.

error: Content is protected !!