January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘ACT-Wazalendo wanamhadaa Nyerere’

Spread the love

CHAMA kipya cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), kimeasisi kauli mbiu ya “kufuata falsafa ya Mwalimu Nyerere.

Miongoni mwa wanachama wake waliojiunga hivi karibuni pamoja na Zitto Zuberi Kabwe ni Jaji mstaafu Musa Kwikima, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Haki za Binadamu Kanda ya Magharibi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Jaji Kwikima alipokuwa kwenye kongamano la wanaharakati wa Kiislamu Tabora, lililofanyika katika uwanja wa Urongoni tarehe 30 Januari 2011, alitambulishwa kuwa ni mmoja wa watu katika nchi hii wasiokubaliana na falsafa ya Mwl. Nyerere wala itikadi yake, kwa sababu hakumteua kuwa Jaji Mkuu wa Tanganyika mara baada ya uhuru.

Akifafanua chuki hiyo kwa Mwl. Nyerere iliyotolewa na Jaji Kikwima, Mzee Bilal Rehani Waikela alisema, “huyu Kwikima baada ya jaji aliyeombwa huko nje kuja kuwa mkubwa hapa, ilikuwa akitoka yeye ndiye awe. Lakini Nyerere alibadilisha, ikampeleke Francis Nyalali shule akasome, amalize aje ashike wadhifa huo.”

Mzee Waikela alisema kuwa Jaji Kwikima alimwita Nyerere “habithi” maana yake mtu mwovu, fisadi na mjanja. Kwamba hata alipopewa kuzungumza, Jaji Kwikima hakukanusha wala hajawahi kukanusha mahali popote kuhusu tuhuma hizo.

Sasa ni lini alipoondoa chuki hiyo dhidi ya falsafa za Mwl. Nyerere hata leo aibukie nazo ACT-Wazalendo?

Wapenda amani wanajiuliza watatofautishaje maneno na matendo ya watu ambao kwa maneno wanasema wanamkubali Mwl. Nyerere huku kumbukumbu zilizopo zikionesha wana chuki kubwa dhidi yake na falsafa zake?

Ikiwa chuki dhidi ya Mwl. Nyerere ya tangu mwaka 1964 imekuja kuibukia mwaka 2011, miaka 47 baadaye, ughafla wa kuipenda falsafa yake umesukumwa na nini?

Wafuasi wa falsafa ya Mwl. Nyerere wanajiuliza maswali mengi kwamba ikiwa hukutubu kwa mtu uliyemkosea alipokuwa hai, je ukitubu baada ya yeye kufa nani ataipokea toba yako?

Tafsiri inayobaki hapo ni mwendelezo ule ule wa roho ya usaliti na unafiki ambavyo Mwl. Nyerere alivipinga kwa nguvu zake zote na ndiyo maana taifa letu likajulikana kwa kuwa na umoja.

Jaji mstaafu Kwikima anayedai amejiunga na ACT-Wazalendo kwa kumfuata Zitto kwa madai ya kufuata falsafa ya Nyerere huku moyoni akiwa na chuki naye ni msaliti na mnafiki.

Mwandishi wa makala haya amejitambulisha kama msomaji wa MwanaHALISIOnline

error: Content is protected !!