July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Wazalendo wamshangaa AG

Ado Shaibu, Katibu Mkuu ACT-Wazalendo

Spread the love

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeshangazwa na hatua ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyobatilisha wakurugenzi kusimamia uchaguzi. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Akizungumza na wanahabari leo tarehe 14 Mei 2019 jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema, hatua ya serikali kukatia rufaa hukumu hiyo inasikitisha kwa kuwa, inakiuka masilahi ya umma na ustawi wake.

Tarehe 10 Mei 2019, Mahakama Kuu ya Tanzania mbele ya Jaji Utuganile Ngwala, ilitoa uamuzi wa kesi ya kikatiba namba 8 ya mwaka 2018 iliyofunguliwa na Bob Chacha Wangwe, kwa kubatilisha kifungu cha Sheria cha 7 (3) kinachoruhusu wakurugenzi wa manispaa a halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Katika uamuzi huo, Mahakama ilitengua kifungu cha 7 (1) kinachoruhusu mtu yeyote kuwa msimamizi wa uchaguzi, ambapo Jaji Ngwala wakati akisoma uamuzi huo alisema sheria hizo ni batili na kinyume cha katiba ya nchi.

Ado ameeleza kuwa, huu ni wakati wa wadau wa demokrasia nchini, vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla, kushikamana kwa pamoja na kupaza sauti zao dhidi hatua ya serikali kuzuia mageuzi katika mfumo wa usimamizi wa uchaguzi kuendana na matakwa ya umma.

“Kauli ya serikali iliyotolewa jana tarehe 13 Mei 2019, kupitia mwanasheria mkuu wa serikali kuwa, serikali imetoa notisi katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kwa kesi Na. 6/2018 inasikitisha sana,” amesema Ado na kuongeza;

“Uamuzi huu na ule wa rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu dhidi ya ndoa ya utotoni (kesi ya Rebecca Gyumi), unadhihirisha kuwa, Serikali ya CCM haipo kwa ajili ya maslahi ya umma wala ustawi wake.”

Aidha, ACT-Wazalendo kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iajiri watendaji wake wenyewe hadi kwenye ngazi za wilaya, waliothibitika kuwa na sifa za uadilifu na wasio wanachama wa chama chochote cha siasa ajili ya kusimamia uchaguzi.

“Kwa sababu sasa Tume inawajibika kuwa na watumishi wake hadi ngazi za chini, uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji nao usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi badala ya TAMISEMI. Kisingizio cha muda mrefu cha uchaguzi huu kusimamiwa na wizara ya TAMISEMI ni kuwa tume haina watendaji hadi ngazi za chini,” amesema Ado.

error: Content is protected !!