Saturday , 13 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa ACT-Wazalendo wamchongea Rais Magufuli kwa wafanyakazi
Habari za Siasa

ACT-Wazalendo wamchongea Rais Magufuli kwa wafanyakazi

Rais John Magufuli akifungua mkutano wa ALAT. Picha ndogo, Ado Shaibu Katibu, Itikadi, Mawasiliano na Uenezi - ACT Wazalendo
Spread the love

CHAMA cha ACT Wazalendo kimeshitaki Rais John Magufuli kwa wafanyakazi kutokana na kauli zake alizozitoa jana alipokuwa akihutubia katika Mkutano wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT), anaandika Faki Sosi. 

ACT-Wazalendo wameziita kauli zilizotolewa na rais Magufuli dhidi ya wafanyakazi ni dharau kwa kada hiyo na kuwataka waamke na kuchukua hatua juu ya kauli hizo.

Katika tamko lililotolewa na chama hicho ambalo limechambua kauli za Rais Magufuli na kutoa msimamo wa chama. Soma taarifa ya ACT-Wazalendo hapa chini.

Wafanyakazi amkeni, kauli ya Rais ni dharau dhidi ya haki zenu

Chama cha ACT Wazalendo kimesikitishwa na baadhi ya kauli zisizo za kiuongozi zilizotolewa jana, Oktoba 3, 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndugu Magufuli, kwenye hotuba yake aliyoitoa kwenye ufunguzi wa mkutano wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT).

Rais alitoa kauli mbalimbali ambazo baadhi zimezua taharuki na kuibua mjadala mkubwa kwenye jamii. ACT Wazalendo tunadhani kwamba baadhi ya kauli hizo haziwezi kupita hivi hivi bila kuwekwa kwenye uhalisia wake.

Tunayafanya haya kwa sababu licha ya ukweli kwamba nchi yetu ni ya utawala wa sheria yenye ukuu wa katiba (Constitutional Supermacy), wapo watu miongoni mwa watawala na ndani ya chama cha CCM wanaishi kifikra kama vile uongozi wa nchi yetu ni wa Kifalme.

ACT Wazalendo tunao wajibu wa kuwakumbusha watu hao juu ya kufuata Katiba ya nchi, kuacha kauli zisizo za kiuongozi, pamoja na kutokujiona ni wafalme wanaoweza kufanya chochote watakacho. Ni imani yetu kuwa tusipowakemea watu wa namna hii kwa kauli husika, wanaweza kuuaminisha umma kuwa kauli husika ndio hali halisi na wakaanza kuzikumbatia mfano wa sheria (hali ambayo imeanza kuzoeleka sasa).

Maelezo yetu yatajikita kwenye masuala Kupandisha Mishahara ya Wafanyakazi wa sekta ya Utumishi wa Umma kama ifuatavyo:

Magufuli ameweka bayana kuwa alipoingia madarakani hakuongeza mishahara ya wafanyakazi na wala hana mpango wa kufanya hivyo kwa sababu yeye hakuchaguliwa kuongeza mishahara na kwamba ana jukumu la kuwahudumia wananchi.

Swali la kujiuliza baada ya kauli hiyo ni: Je wafanyakazi wa Tanzania wanastahili kufanyiwa hivi na serikali wanayoihudumia? Jibu bila Shaka ni hapana. Serikali inatoa wapi ujeuri wa namna hii dhidi ya wafanyakazi nchini wakati kiuzalishaji na kimapato inawategemea Wafanyakazi?

Licha ya mchango wao madhubuti katika ujenzi wa Taifa kwenye sekta mbalimbali, kwa utumishi wao wa kutukuka, ukweli wa mambo ni kuwa wafanyakazi ndio wanaochangia zaidi mapato ya serikali kuliko waajiri wao.

Kwa mfano, Kitabu cha Mapato ya Serikali Kuu cha mwaka 2016/17 kinaonyesha kuwa Wafanyakazi wote wa sekta ya Umma na Sekta Binafsi watachangia jumla ya shilingi trilioni 3 kwenye mapato yote ya Serikali kulinganisha na wenye mitaji (waajiri) ambao watachangia jumla ya shilingi bilioni 900 tu kutoka kwenye kodi za faida/gawio, ongezeko la mitaji na riba (taxes on income/interests, profits and capital gains).

Hata ukitazama miaka miwili ya nyuma utaona kwamba mwaka 2015/16 makampuni yalichangia shilingi 773 bilioni wakati Wafanyakazi walichangia shilingi 2.2 trilioni na mwaka 2014/15 makampuni yalichangia shilingi 600 bilioni na wafanyakazi shilingi 1.9 trilioni kama kodi zao kwenye mapato ya Serikali.

Kwa kutumia kigezo cha Kodi za Mapato, waajiri wanachangia robo tu ya mapato yote ya serikali na wafanyakazi wanachangia robo tatu iliyobakia. Hivyo basi, kutokana na mchango wao, ingetazamiwa kwamba mkuu wa nchi angetanguliza mbele maslahi yao hasa ulipwaji wa mishahara bora badala ya kuyapuuza.

Kwanini Serikali inawadharau na kuwahadaa Wafanyakazi namna hii? Wakati wa kampeni za kugombea Urais, Magufuli alijipambanua mbele ya Watanzania kuwa akichaguliwa kuingia madarakani, Serikali itahakikisha kuwa inasimamia maslahi bora ya wafanyakazi ikiwemo mishahara bora.

Rais alitoa ahadi hii kimkakati akijua kwamba wafanyakazi wanao mtaji mkubwa wa kura. Ahadi hiyo ilirejewa hivi karibuni kwenye sherehe za Mei Mosi 2017 ambapo Rais aliwahakikishia wafanyakazi kwamba kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018, serikali yake itahakikisha ongezeko la mishahara kwa wafanyakazi, na Waziri wake, ndugu Angellah J. Kairuki ameomba Bunge kuidhinisha shilingi bilioni 650 kwa mwaka wa fedha 2017/18 kwaajili ya nyongeza hiyo.

Kauli ya jana ya Rais ni mfano dhahiri wa hadaa dhidi ya wafanyakazi nchini. Kauli hii inaonyesha kiburi na dharau kubwa mno dhidi ya wafanyakazi nchini, ni kauli ya mtu asiyeheshimu ilani ya uchaguzi wa chama chake, ahadi ya kampeni ya Urais aliyoitoa mwenyewe, ahadi aliyoitoa katika maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) mwaka huu, pamoja na maamuzi yaliyopitishwa na Bunge letu tukufu yatokanayo na maombi ya kasma ya kibajeti ya Wizara iliyo chini yake (Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma).

Mapendekezo ya ACT Wazalendo:

1. Ongezeko la mshahara ni haki ya msingi ya wafanyakazi. ACT Wazalendo inaitaka Serikali itekeleze mara moja wajibu wake kwa wafanyakazi.

2. Huu ni wakati wa vyama vya wafanyakazi kushikamana zaidi. Ni muhimu vyama vya wafanyakazi hasa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kufahamu kuwa serikali ya sasa HAINA mpango wa kuwapatia wafanyakazi haki zao, na inawadharau. TUCTA ina wajibu wa kusimama imara kuzipigania haki hizo. Daima, haki hupiganiwa. ACT Wazalendo tuko tayari kushirikiana na TUCTA katika kuwaunganisha Wafanyakazi kupigania haki zao.

3. Ni muhimu kwa wafanyakazi Wote kuzikumbuka dharau hizi za serikali hizi kwao. Kauli hizi za kuwadharau wafanyakazi zitumike kama tiketi ya kuiweka kando serikali isiyo na utu ya CCM katika uchaguzi mkuu.

Ado Shaibu
Katibu, Itikadi, Mawasiliano na Uenezi – ACT Wazalendo
Oktoba 4, 2017
Dar es salaam

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Nchimbi aanika ugonjwa wa CCM

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emanuel Nchimbi,...

Habari za Siasa

Chadema yapuliza kipyenga uchaguzi viongozi kanda

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza maandalizi ya uchaguzi...

Habari za Siasa

CCM :Hatutaki ushindi wa makandokando uchaguzi Serikali za mitaa

Spread the loveCHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakihitaji ushindi wa makandokando katika...

Habari za Siasa

Makala: Puuzeni wanasiasa wanaojigamba wanaweza kubadili maamuzi ya mahakama

Spread the loveKATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),...

error: Content is protected !!