May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Wazalendo waitetea kauli ya Halima Mdee

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT

Spread the love

NGOME ya Vijana ya chama cha ACT-Wazalendo, imesema kuna hatari ya utawala wa sheria nchini kuporomoka endapo watanzania hawatapigania sheria na amani ya nchi, anaandika Hamisi Mguta.

Hayo yameelezwa leo na Karama Kaila, Mwenezi wa Ngome ya Vijana ya chama hicho, katika tamko lao ikiwa ni siku nne tangu kukamatwa kwa Halima Mdee, Mbunge wa Kawe (Chadema) kwa amri ya Ally Hapi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC).

“Tukumbuke kuwa wazee wetu waliopigania uhuru wa nchi hii hawakufanya hivyo kumuondoa mtu mwenye ngozi nyeupe, bali walifanya hivyo wakitarajia kuondoa kila aina ya uonevu dhidi yao ikiwemo kubanwa kwa uhuru wa kujieleza na kujiamulia mambo yao bila kuvunja sheria,” amesema Kaila.

Karama Kaila, Mwenezi wa Ngome ya Vijana ya chama cha ACT-Wazalendo

DC Hapi aliagiza Mdee akamatwe na kuwekwa ndani kwa saa 48 Julai 4 kwa kudai kuwa alitoa maneno ya kukashifu na ya uchochezi katika mkutano wake wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) uliofanyika Julai 3 makao makuu ya chama hicho alipozungumza kuhusu msimamo wao kwa wanafunzi waliopata mimba kurudi shuleni.

Kaila amesema baadhi ya wateule wa rais wamegeuza kauli mbalimbali kutoka kwa rais kama sehemu ya kuwakomoa wenye mawazo tofauti na kauli au matakwa ya rais, huku akisisitiza kuwa misingi ya utawala bora ni kuheshimu katiba ya nchi ambayo ndiyo sheria mama.

“Amri ya mkuu wa wilaya ya kinondoni kuamuru kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa mbunge wa Kawe ni matumizi mabaya ya sheria na uvunjifu wa katiba ya nchi ambayo viongozi wa umma wameapa kuilinda na kuisimamia.

“Tunasema hivi kwa sababu Mdee hakumtukana rais wala hajatoa maneno yoyote yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kama anavyodai DC Alli Hapi,” amesema Kaila.

error: Content is protected !!