August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ACT Wazalendo waitaka Serikali kushughulikia migogoro ya wakulima, wafugaji

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu Ado

Spread the love

CHAMA cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuchukua hatua za dharura kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji ili kuzuia maafa yanayoweza kutokea. Anaripoti Mwandishi Wetu, Lindi … (endelea).

Wito huo umetolewa jana tarehe 09 Julai 2022 na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu Ado akizungumza na Wanachama na Viongozi wa ACT Wazalendo katika Kata ya Kikole katika Jimbo la Kilwa Kusini Wilayani Kilwa.

Alisema migogoro ya wakulima na wafugaji ni sawa na bomu linalosubiri kulipuka.

“Tayari migogoro hii imeshaleta maafa kwenye maeneo mengi Nchini ikiwemo kutokea kwa mapigano makali baina ya wafugaji na wakulima. Hata hapa Kata ya Kikole nimeelezwa kuwa kuna mapigano yametokea leo na kuna mtu mmoja amefariki . Serikali isipochukua hatua za haraka, maafa makubwa zaidi yatayokea,” alisema Ado.

Alisema ili kutatua migogoro hiyo, serikali inatakiwa kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi.

“Yatengwe maeneo ya Wakulima na wafugaji na pasiwe na muingiliano. Mathalani, katika Mkoa wa Lindi, ardhi inayofaa kwa kipimo ni hekta 1,000,000 huku zilizotumika ni hekta 400,000 sawa na 40% upande wa mifugo, hekta zinazofaa kwa mifugo ni hekta 450,000 huku zilizotumika zikiwa hekta  22,000 sawa na  5% tu. Hivyo basi, mkoa wa Lindi hauna shida ya ardhi kwa ajili ya ufugaji na kilimo. Kinachokosekana ni mipango mizuri ya matumizi ya ardhi” alisisitiza Ado.

Pia alisema ni lazima wananchi wa vijiji husika wasikilizwe na maamuzi yao yaheshimiwe.

“Mathalani, nimeelezwa kuwa hapa kuwa katika Kijiji cha Kikole, hakuna sehemu iliyotengwa kwa ajili ya wafugaji, lakini mifugo mingi inaingizwa na kuharibu mazao. Nani anayeruhusu mifugo hiyo?

“Ni dhahiri hapa patakuwa na mtandao wa rushwa inayonufaisha viongozi.  Ni lazima Waziri Mwenye dhamana ya mifugo awajibike kwa kuchukua hatua kumaliza tatizo hili. La sivyo, ACT Wazalendo tutakuja na kampeni kumtaka Waziri wa Mifugo Abdallah Ulega ajiuzulu kama suala hili la migogoro ya wafugaji na wakulima halitopatiwa ufumbuzi” aliongeza Ado.

Katibu Mkuu huyo wa ACT Wazalendo akiambatana na Katibu wa Sera na Utafiti, Idrisa Kweweta yupo kwenye ziara ya Kata kwa Kata kwenye Jimbo la Kilwa Kusini yenye lengo la kuhakiki uhai wa Chama, kuhamasisha usajili wa Wanachama kwenye Mfumo wa ACT Kiganjani na kutoa mwelekeo wa kisiasa wa Nchi ikiwemo kufafanua jitihada ambazo ACT Wazalendo inazichukua katika kupigania Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.

Ziara hiyo iliyoanza tarehe 08 Julai 2022 inatarajiwa kuisha tarehe 13 Julai 2022.

error: Content is protected !!