CHAMA cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania kimesema, kimeshtushwa na kifo cha mwenyekiti wake, Maalim Seif Sharif Hamad, kilichotokea leo Jumatano tarehe 17 Februari 2021, kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema, chama hicho kimepata pigo kubwa kwa kuondokewa na kiongozi wake.
Zitto amesema, hakuna maneno ambayo anaweza kuyaelezea kuhusu kifo cha Maalim Seif (77), kwa kuwa Mungu mwenyewe amemua kumchukua mja wake.
“Hakuna maneo ambayo, tunaweza kuyaeleza kwa wanachama, Wazanzibar na kwa Watanzania kwa ujumla kuhusiana na uchungu mkubwa wa taarifa hii, lakini sisi sote ni wa Mungu na kwake tutarejea,” amesema Zitto kwa uchungu mkubwa.
Akizungumza kwa upole, Zitto amesema, alikwenda Muhimbili asubuhi ya leo kwa ajili ya kumjulia hali Maalim Seif, na kwamba alielezwa na jopo la madaktari waliokuwa wanamuangalia mwanasiasa huyo, kwamba hali yake kiafya inaonyesha matumaini.
“Kwa mujibu wa taarifa ya madaktari na leo asubuhi nilikuwa hospitalini mpaka saa 2.00 asubuhi, nilikuwa hospitalini Muhimbili na kuzungumza na jopo la madaktari waliokuwa wanamhudumia na hali yake ilikuwa inatia matumaini.”

“Hata hivyo, mnano saa 5:26 asubuhi, mwenyezi Mungu alitwaa roho yake,” amesema Zitto
Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo amesema, taratibu za mazishi zitatolewa baada ya kuwasiliana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Leave a comment