May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi walaani kushikiliwa Mbowe na wenzake, wasema…

Zitto Kabwe kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo

Spread the love

 

VYAMA vya siasa vya upinzani nchini Tanzania vya NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo, vimeiomba Serikali nchini humo kukaa pamoja na vyama vya siasa, kwa ajili ya kupata muafaka wa njia nzuri ya kufanya siasa bila uhasama. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Wito huo umetolewa leo Ijumaa, tarehe 23 Julai 2021 kupitia tamko la pamoja lililotolewa na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia kuhusu kukamatwa na kushikiliwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake 11.

Mbowe anatuhumiwa na polisi kwa tuhuma za kupanga njama za kutaka kufanya mauaji ya viongozi wa serikali pamoja na ugaidi.

“Tunatoa wito kwa viongozi wa Serikali na viongozi wa vyama vya siasa nchini, kuwa tukae chini tuzungumze namna njema ya kufanya siasa bila uhasama. Ni wakati sasa wa viongozi kuzungumza (political dialogue),” limesema tamko la viongozi hao.

Mbowe na wenzake 11, walikamatwa saa 8 usiku wa kuamkia tarehe 21 Julai 2021, wakiwa katika Hoteli ya Kingdom jijini Mwanza.

Baada ya kuhojiwa jijini Mwanza, Mbowe alisafirishwa kuelekea jijini Dar es Salaam.

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi 

Vyama hivyo vimetoa wito kwa Jeshi la Polisi, kumuachia mara moja Mbowe na wenzake 14 ambao wanashikiliwa jijini Mwanza kwa tuhuma hizo.

“Hivyo basi, kwa niaba ya vyama vya NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo, tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kuwaachia mara moja bila masharti viongozi wote wa Chadema, wakiongozwa na Mbowe,” limesema tamko hilo.

Vyama hivyo vimesema, hatua ya Mbowe kukamatwa inafifisha utengamano wa nchi “aidha, tunatoa rai kwa watu wote wenye mapenzi mema, kukemea hali hii ambayo inafifisha zaidi utengamano katika nchi.”

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Mbowe na wenzake akiwemo Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema, John Pambalu. Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, John Heche na Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Walikamatwa kwa tuhuma za kutaka kufanya kongamano la kudai katiba mpya bila kibali. Kongamano hilo lilipangwa kufanyika Jumatano iliyopita, jijini Mwanza.

Lakini lilizuiwa kwa kigezo cha kuzuia mikusanyiko kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Corona.

error: Content is protected !!