CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimemlilia aliyekuwa mwenyekiti wake wa kwanza, Anna Mghwira, kikisema kwamba kifo chake kimeacha pigo katika medani za kisiasa nchini Tanzania. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 22 Julai 2021 na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma ACT-Wazalendo, Janeth Rithe.
Saa kadhaa baada ya mwanasiasa huyo kufariki dunia, katika Hospitali ya Mount Meru, jijini Arusha, alipokuwa anapatiwa matibabu.
“Taifa limempoteza kiongozi mwenye upeo na uwezo mkubwa wa masuala mbalimbali. Pamoja na kwamba hakuwa mwanachama wala kiongozi, katika chama chetu mpaka umauti unamkuta, historia yake kwetu iliacha alama zisizofutika,” imesema taarifa ya Rithe.
Mghwira alikuwa mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, kuanzia 2015 hadi 2017, alipojiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), tarehe 8 Disemba 2017, baada ya kuteuliwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Rais Magufuli aliyefariki dunia akiwa madarakani tarehe 17 Machi 2021, alimteua Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, mwezi Juni 2017, akimtoa katika chama cha ACT-Wazalendo, alikokuwa mwenyekiti.
Taarifa ya Rithe imesema, ACT-Wazalendo itautambua na kuuenzi mchango wake, alioutoa kupitia uongozi wake akiwa mwenyekiti wa chama hicho.
“Mama Mghwira alikuwa Mwenyekiti wa kwanza wa ACT Wazalendo, mara baada ya chama kupata usajili wa kudumu kuanzia mwaka 2015 hadi 2017. Chama kitautambua mchango na uongozi alioutoa akiwa mwenyekiti,”imesema taarifa ya Rithe.
Mbali ya kuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Mghwira alikuwa mgombea wa chama hicho katika nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Leave a comment