April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

ACT- Wazalendo kimenuka, ‘swahiba wa Zitto’ aachia ngazi

Spread the love

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Msafiri Mtemelwa, ametangaza kujiuzulu nyazifa zake, kufuatia kuvuja kwa mazungumzo yake na mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu. Anaandika Hamis Mguta…(endelea).

Akizungumza katika ofisi za MwanaHALISI, leo Jumapili, tarehe 15 Desemba 2019, Mtemelwa aambaye ni mmoja wa wanasiasa wakongwe nchini alisema, ameamua kujiuzulu nyadhifa hizo za uongozi, ili kuwabika kwa kilichotokea.

“Mazungumzo yetu yalikuwa ya faragha sana. Nawajibika kwa kuvuja kwa mazungumzo hayo, wakati yalikuwa bado hayajaiva,” ameeleza Mtemelwa.

Amesema, audio inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, inalengo la kumgombanisha yeye na chama chake, yeye na viongozi wenzake, pamoja na wanachama na wafuasi wa ACT- Wazalendo, “waliotapakaa nchi mzima.”

Mtemelwa anakiri kuwa alifanya mazungumzo na Komu, yenye lengo la kumshawishi mwanasiasa huyo, kujiunga na chama chake.

Hata hivyo, anasema kuwa baadhi ya yaliyomo kwenye video hiyo, yamehaririwa kwa kiasi kikubwa na watu anaodai kwua wana lengo baya dhidi ya ACT- Wazalendo na viongozi wake.

Amesema, “kwenye audio inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, inayonihusisha mimi, Zitto Zuberi Kabwe, Maalim Seif Shariff Hamad na watu wengine, imetengenezwa kwa nia ovu ya kutaka kukivuruga ACT-Wazalendo.”

                         Maalim Seif Hamad, Mshauri wa Chama cha ACT-Wazalendo

Anasema, “ni ukweli usio na shaka kwamba maneno hayo yaliyoingizwa kwenye audio hiyo, yamewekwa kwa nia ovu ya kunigombanisha mimi na chama changu; na mimi na viongozi wangu; na kazi hii chafu, imefanywa na watu wenye nia mbaya na chama chetu.

“Mimi binafsi, sijawahi hata mara moja kumvunjia heshima Maalim Seif, kwa kuwa ni mtu ninayemheshimu sana. Amejitolea muda wake mwingi kujenga demokrasia katika nchi yetu, na kwa nafasi alizoshika na hadhi aliyonayo, ni vitu ambavyo havifanani na kwa mtu anayemjua kama mimi, nisigeweza kusema maneno ya aina hiyo.”

Akimzungumzia Maalim Seif, Mtemelwa anasema: “Kwangu mimi, Maalim Seif amekuwa mwalimu wangu wa siasa, baba, rafiki na mlezi na katika kipindi nilichokuwa naye karibu, nimegundua yanayosemwa juu yake, ni tofauti na yeye anavyoishi.

“Ninamheshimu sana Zitto kutokana na historia yetu ya mageuzi na tulikotokea. Nafahamu madhara ya migogoro kwenye vyama, hasa vyama hivi vyetu ambavyo havijawahi kushika madaraka ya nchi. Kwa hivyo, kwa vyovyote vile, nisigeweza kuzungumza maneno hayo kama yanavyonukuliwa.”

Alipoulizwa kutokana na kadhia hiyo ameamua kuchukua hatua gani, Mtemelewa anasema, “kwanza, namuomba radhi Maalim Seif na familia yake; namuomba radhi Zitto, naiomba radhi Kamati Kuu (CC) ya chama changu.

                                         Anthony Komu, Mbunge wa Moshi Vijijini

“Si hivyo tu: Nawaomba radhi wanachama wenzangu, washabiki wa ACT – Wazalendo popote waliko ndani na nje ya nchi na watu wote wanaoamini katika demokrasia.”

Aidha Mtemelwa anasema, “kutokana na taharuki iliyotokea na kwa manufaa ya chama changu, nimeamua kujiuzulu nyadhifa zangu zote ndani ya chama, ikiwamo naibu katibu Mkuu (Bara) na Mjumbe wa Kamati Kuu, ili kuwajibika na kuonyesha umma kuwa mambo yaliyotokea, hayakuwa na nia mbaya.”

Anasema, tayari ameijulisha ofisi ya katibu mkuu kuhusiana na maamuzi yake hayo.

Katika audio ambayo imemsababishia Mtemelwa ameamua kujiuzulu, mwanasiasa huyo anasikika akimwambia Komu kuwa ajiunge na chama chake ili aweze kuwa katibu mkuu; huku yeye Mtemelwa akidaiwa kuwakandia baadhi ya viongozi wake.

Komu hakupatikana kuzungumzia suala hilo. MwanaHALISI linaendelea kumtafuta.

error: Content is protected !!