August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Wazalendo: CCM ikileta Katiba pendekezwa tutahamasisha wananchi waikatae

Spread the love

CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimesema endapo Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitatumia Rasimu ya Katiba Pendekezwa katika mchakato wa upatikanaji Katiba mpya, watahamasisha wananchi waikatae kupitia kura ya maoni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tanga…(endelea).

Onyo hilo limetolewa leo Jumamosi, tarehe 23 Julai 2022 na Kaimu Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Ismail Jussa, akiwasilisha mada katika kongamano la chama hicho la tume huru ya uchaguzi kuelekea katiba mpya, lililofanyika jijini Tanga.

Jussa amesema kuwa, ACT-Wazalendo haiungi mkono rasimu ya katiba pendekezwa kwa kuwa ina baadhi ya masuala ambayo hawayaungi mkono, ikiwemo muundo wa Serikali, madaraka ya Rais na mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili ya nchi.

“CCM wanatajataja katiba pendekezwa, tumewaambia waziwazi wakileta katiba pendekezwa tutawahamasisha umma kama tulivyohamasisha wakati ule kuikataa katiba pendekezwa kupitia kura ya maoni,” amesema Jussa.

Jussa amesema kuwa, ACT-Wazalendo kinaunga mkono Rasimu ya Katiba ya Jaji Mstaafu, Joseph Warioba, iliyotokana na maoni ya wananchi na kwamba kama CCM kuna baadhi ya masuala yaliyomo katika rasimu hiyo haiungi mkono, mjadala wa kitaifa ufanyike ili kutafuta muafaka.

“CCM ni sehemu ya nchi hivyo wana haki yao, yale maeneo ambayo tumebishana ambayo hawaridhiki nayo kwenye rasimu ya Jaji Warioba na sisi tuna maeneo kwenye katiba pendekezwa hatuafikiani nayo. Tunasema mkutano wa kitaifa urejeshwe ili maeneo tunayobishana tukajadiliane mpaka tupate muafaka wa kitaifa kwenye maeneo yote,” amesema Jussa.

Mwanasiasa huyo amesema kwa sasa mvutano uliokuwepo kuhusu katiba pendekezwa ni muundo wa Serikali ambapo katiba pendekezwa inapendekeza muundo wa Serikali mbili, wakati rasimu ya Jaji Warioba ikipendekeza muundo wa Serikali tatu, ya Zanzibar, Tanganyika na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jussa amesema, mvutano mwingine ni kuhusu madaraka ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

“Eneo la pili ni madaraka ya Rais, sisi tunasema katiba tunayotumia inalimbikiza madaraka makubwa mno kwa Rais na nyie mnaona uteuzi lazima ufanywe na Rais hata wa watendaji wa mihili inayojitegema unafanywa na Rais,” amesema Jussa.

Jussa amesema “hata katibu wa Bunge anateua Rais, majaji wa mhimili mwingine wanateuliwa na Rais. Katiba imempa madaraka Rais kwamba ahojiwi, halazimiki kufuata ushauri wa mtu yeyote na hashtakiwi kwa mambo aliyotenda kabla na baada ya kuwa Rais. Hatuwezi kuwa na katiba inayomfanya Rais kuwa Mungu mtu maana asiyekosea ni Mungu tu.”

error: Content is protected !!