Thursday , 18 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa ACT-Wazalendo: 2022 mchungu kwa wanyonge, raha kwa vibonge
Habari za SiasaTangulizi

ACT-Wazalendo: 2022 mchungu kwa wanyonge, raha kwa vibonge

Waziri Mkuu Kivuli wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu
Spread the love

 

IKIWA zimesalia siku tatu kufika tamati ya mwaka 2022, Chama cha ACT-Wazalendo kimeutaja mwaka huo kuwa wa misukosuko, “mchungu kwa wanyonge na raha kwa vibonge,” kutokana na matukio mbalimbali yaliyojitokeza ambayo yameathiri maisha ya wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, tarehe 28 Desemba 2022 na Waziri Mkuu Kivuli wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu akitoa tathimini ya Kamati ya Kusimamia Serikali ya chama hicho, kuhusu mambo yaliyotokea katika kipindi cha mwaka mzima.

“Kamati ya Kusimamia Serikali ya ACT-Wazalendo, tumeuona 2022 ni mwaka wa misukosuko, chungu kwa wanyonge raha kwa vibonge,” amesema Semu.

Semu ambaye pia na Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Bara, amesema mwaka huo ulikuwa wa misukosuko kwa wananchi kutokana na hali ngumu ya maisha kwa wananchi iliyotokana na mfumuko wa bei za bidhaa.

Amesema, kufuatia hali hiyo ngumu ya maisha, ACT-Wazalendo kupitia kamati hiyo ilipigania masuala mbalimbali yaliyowagusa wananchi, ikiwemo mwenendo wa uchumi na kupanda gharama za maisha, ambapo iliishauri Serikali kuchukua hatua za makusudi na za haraka kukabiliana nayo.

“Tumeshuhudia kupanda kwa bei za mafuta ya petroli, diseli na mafuta ya taa. Pili, bidhaa za chakula kama vile Maharage, Mafuta ya kula, Sukari, unga na Mchele vimepanda zaidi ndani ya mwaka mmoja. Vilevile, kupaa kwa pembejeo za kilimo na Mbolea,”

“Baada ya kupaza sauti na kutoa mapendekezo kwa Serikali kuweka ruzuku kidogo imeshuka. Tatu, kupanda kwa vifaa vya Ujenzi kama vile Saruji, bati, nondo Tatu, wakati tunashuhudia kupanda kwa gharama za maisha kwa upande mmoja, upande mwingine tunaona kutetereka kwa bei za mazao ya kilimo kama vile Tumbaku na Korosho,” amesema Semu.

Aidha, Semu amesema mwaka huo ulikuwa wa misukosuko kutokana na majanga yaliyotokea ikiwemo ajali ya treni iliyotokea Tabora, ajali ya ndege ya Precision Air ya Kagera, ajali ya moto ulioteketeza Mlima Kilimanjaro, pamoja na ajali za moto katika masoko ya wafanyabiashara wadogo, ambapo kamati hiyo pia ilitoa maependekezo kwa Serikali juu ya namna ya kukabiliana nayo na kutoa ahueni kwa wahanga.

“Tulitoa pendekezo la kupunguza tozo, ushuru na kodi kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ambazo ni muhimu kwa maisha ya watu kama vile mafuta ya kula, sukari, ngano na mafuta ya petroli na Diseli. Na kuongeza uzalishaji wa chakula na mahitaji muhimu kwa nchi yetu huku Serikali kuongeza umakini wa kudhibiti soko holela la nje (usafirishaji wa chakula nje) kwa ajili ya kukabiliana na kupanda kwa bei za bidhaa za chakula,” amesema Semu.

Semu amesema “licha ya hapa na pale Serikali ilitekeleza baadhi ya mapendekezo tuliyowahi kutoa japo sio kwa ufanisi na kwa usahihi, kama vile ilitoa ruzuku ya mafuta na mbolea, kuondoa kodi kwenye mafuta ya kula na kupunguza tozo za miamala ya kieletroniki (Simu na Benki).”

Akitaja mambo mengine yaliyofanywa na ACT-Wazalendo kwa 2022, Semu amesema walisimamia miswada mbalimbali ya sheria na kanuni zilizoenda bungeni ikiwemo Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote, ambao Bunge liliahirisha kuusoma kwa mara ya pili kwa ajili ya Serikali kufanya marekebisho kuhusu dosari zilizotajwa na wadau ikiwemo chama hicho.

Amesema jambo lingine lililopiganiwa na ACT-Wazalendo ni kanuni ya kikokoto cha mafao ya uzeeni ambapo ilipambana kuhakikisha hazipitishwi na Bunge kwa kutoa mapendekezo mbadala kwa lengo la kuondoa masharti yanayopunja mafao wastaafu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia kutunukiwa udaktari wa heshima Uturuki

Spread the loveBaraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia atua Uturuki kwa ziara ya siku 5

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan leo Jumatano amewasili nchini Uturuki kwa...

Habari za SiasaTangulizi

Samia arejesha mikopo ya 10%, bilioni 227.96 zatengwa

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amerejesha utaratibu wa utoaji mikopo...

Habari za Siasa

Rais Samia amfariji mjane wa Musa Abdulrahman

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan leo Jumanne amempa pole Mwanakheri Mussa...

error: Content is protected !!