January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ACT-Tanzania: Demokrasia au ufalme wa Zitto?

Zitto Kabwe akikabidhiwa kadi ya ACT-Wazalendo

Spread the love

KINACHOJIITA chama kipya cha siasa nchini – ACT Tanzania na ambacho kilizinduliwa jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita, kimepoteza upya wake. Kimekumbatia ukale.

Viongozi wake ni wale walioshindwa kufanya kazi za kisiasa ndani ya vyama vingine vya upinzani, hususani Chadema.

Wapo waliofukuzwa kwa makosa mbalimbali, yakiwamo usaliti, kushirikiana na maadui wa chama, kushindwa kukisaidia chama kutimiza malengo yake; na kusababisha migogoro huko walikotoka.

Wengine walijifukuzisha na hata kujifukuza wenyewe, baada ya kuona wameshindwa kutekeleza kile walichotumwa ndani ya Chadema, ambacho ni kuhujumu kimbilio na ngome ya wananchi.

Wapo pia, waliogeuza uongo, ubinafsi, ghiliba na usaliti, kuwa ndiyo mtaji wao mkuu wa kila siku wa kufanya shughuli za kisiasa.

Haya yanathibitishwa na hotuba mbalimbali za siku ya uzinduzi wa ACT; kauli za anayeitwa, “Kiongozi Mkuu wa chama,” Zitto Zuberi Kabwe;” pamoja na “falsafa mpya ya chama;” jina la chama na kauli mbiu yake.

Kwa mfano, Zitto anasema, amejiunga na ACT kwa kuwa huko ndiko kunakaoendana na kile ambacho yeye amekuwa akikipigania kwa miaka yote tangu anze siasa. Amekiita, “maslahi ya taifa mbele dhidi ya kitu kingine chochote.”

Amesema amejiunga na chama hicho kuwa ndiyo chama pekee nchini kinachokubaliana na Itikadi ya Ujamaa na kinaamini katika Falsafa ya Nyerere.

Akadai kuwa chama chake kimeamua kulirejesha Azimio la Arusha ambalo liliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere zaidi ya miaka 40 iliyopita.

Aidha, Zitto amesema, amejiunga na chama hicho kwa kuwa ndicho kinachoamini katika msingi wa uadilifu na kimeweka miiko ya maadili ya uongozi na kuhakikisha viongozi wake wote wanakubaliana nayo na kuisaini.

Amedai kuwa ndani ya ACT hakujengwi mtu, bali kunajengwa chama. Kinachowaunganisha ndani ya chama, ni undugu wao na uzalendo wao.

Akarejea tena wimbo wake wa miaka mingi, kuwa miaka 10 ya ubunge wake, ameangusha serikali mara kadhaa, ikiwamo mkataba wa madini wa Buzwagi na ukwapuaji katika sakata la Escrow.

Ni muhimu kujadili hatua kwa hatua ili kubainisha uongo wa mwanasiasa huyu na uwakala wa chama chake.

Kwanza, ni muhimu Zitto afahamu mapema anataka kuwadanganya, wanaomfahamu vizuri. Matendo yake na kauli zake, bado zimerokodiwa na ndivyo vinavyotumika kuelezea ukweli halisi.

Hakujiunga na ACT kutokana na chama hicho kuendana na dhamira yake ya kupigania maslahi ya taifa. Siyo kweli.

Amejiunga na chama hicho baada ya kufukuzwa ndani ya Chadema kutokana na tuhuma za usaliti na kushirikiana na maadui wa chama; naye kukiri kutaka kufanya mapinduzi ya uongozi ndani ya chama – kinyume cha taratibu, katiba na kanuni za chama.

Amejiunga na ACT baada ya mpango wake wa kuvuruga Chadema kukwama. Amejiunga na ACT baada ya kushutukiwa na viongozi wenzake ndani ya Chadema kuwa anatumiwa na anatumika.

Rekodi za mawasiliano yake na Jack Zoka, aliyekuwa naibu mkurugenzi wa usalama wa taifa (TISS); na andishi waliloliandaa na wenzake – Prof. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba – ambalo walilipachika jina la “Mkakati wa Mabadiliko,” yanathibitisha yote haya ninayoandika.

Kama Zitto asingefukuzwa Chadema, asingetoka. Asingedai kuwa Chadema hakina demokrasia. Asingeeleza kuwa yeye ni mfuasi wa Nyerere.

Kama alikuwa haamini kuwa Chadema hakiwezi kutekeleza kile anachoamini, kwa nini alibaki ndani ya chama hicho hadi kufukuzwa? Kwa nini aling’ang’ania uongozi – naibu katibu mkuu na naibu kiongozi wa upinzani bungeni? Kwa nini alikwenda mahakamani kupinga kuhojiwa usaliti wake?

Pili, kauli ya Zitto kwamba amejiunga na ACT kwa kuwa chama hicho ndiyo pekee nchini kinachokubaliana na Itikadi ya Ujamaa na kinaamini katika Falsafa ya Nyerere, haina ukweli. Imelenga kudanganya umma.

Azimio la Arusha, liliuawa na Halmashauri Kuu ya CCM kule Zanzibar, wakati Nyerere akiwa bado hai. Aliwashangaa na hakuonyesha makeke. Kama kuna wa kulirejesha, ni CCM walioliua.

Zitto anaweza kusema tu kwamba “anadandia Azimio la Arusha” na siyo kulirejesha, kwani hakuwa nalo katika ACT na hivyo hawezi kulirejesha ACT.

Aidha, Zitto mwenyewe siyo mjamaa; na kwa namna yoyote ile, hawezi kufanana na Nyerere. Kujaribu kujifananisha naye, ni kujikweza. Hakukubaliki.

Nyerere alikuwa na maono. Lakini hakuwa msaliti. Alichokisema ndicho alichomaanisha. Alitenganisha yake binafsi na yale ya chama chake na rafiki zake. Kwake, uongozi wa umma ulikuwa utumishi; siyo kujikweza au kujinufaisha binafsi.

Katika kipindi chake chote cha uongozi na hata baada ya kung’atuka madarakani, bado alijitahidi kutojiingiza katika mgongano wa maslahi. Zitto hajaweza na wala haitatokea kuweza. Mifano ipo.

Angalia mfano huu: Anayejiita “Nyerere” ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (PAC). Lakini ni huyohuyo anaishi katika nyumba inayomilikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), huko Tabata jijini Dar es Salaam.

Kampuni ya Zitto inayoitwa Leka Dutigite Limited; ilichotewa zaidi ya Sh. 500 milioni na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA).

Mamilioni haya ya shilingi za walipakodi yalilipwa kwa kampuni ya Zitto katika mazingira yaliyosheheni rushwa, upendeleo na mgongano wa maslahi.

Kwa mujibu wa nyaraka kutoka kwa Wakala wa Usajili wa Kampuni na Leseni (BRELA), kampuni ya Leka Dutigite Limited, imesajiliwa 13 Agosti 2012. Mmoja wa wanahisa wake, ni kampuni ya Gombe Advisors Ltd ya Dar es Salaam.

Akaunti za kampuni hii ambazo ziliingiziwa fedha na mashirika hayo ya umma, ni 0150357447800 iliyoko benki ya CRDB, tawi la Pugu Road, Dar es Salaam.

Wakurugenzi wa Gombe Advisors Ltd ni Zitto Kabwe, ambaye kazi yake inatajwa kuwa mchumi na Raphael Ongangi ambaye amekuwa akijitambulisha kama msaidizi wa Zitto.

Zitto, ambaye amekuwa mbunge anabanwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inayomtaka kutaja mali zake zote.

Sasa huyu ambaye anataka aonekane mwenye “Falsafa ya Nyerere,” hakuwahi kutangaza maslahi yake katika mikataba ya Gombe Advisors Ltd, Leka Dutigite Ltd, NSSF na Tanapa.

Kwa muda wote ameshindwa kujibu madai kuwa amefanya biashara na Tanapa – shirika la umma analolisimamia akiwa mbunge na mwenyekiti wa PAC.

Si hivyo tu. Zitto anayetaka kujifananisha na Nyerere amekuwa akidaiwa kulipiwa na taasisi za umma ambazo zinasimiwa na PAC, gharama za usafiri, chakula na malazi katika hoteli mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Zitto huyuhuyu amedaiwa kulipiwa gharama za malazi na chakula katika hoteli ya Mount Meru, mkoani Arusha. Amesafirishwa hadi nchini Rwanda na kulipiwa gharama za siku 10, wakati aliishi huko kwa siku tatu. Rekodi zipo.

Hadi hapo, iko wapi sura ya Nyerere katika matendo haya? Uko wapi uadilifu anaodai kuubeba? Havipo!

Tatu, Zitto amesema, ndani ya ACT hakujengwi mtu; kunajengwa chama; na kwamba kinachowaunganisha, ni undugu wao na uzalendo wa kutetea ukandamizaji wa vyama vingine. Hili nalo siyo la kweli.

Kama ndani ya ACT hakujengwi mtu, kusingekuwa na mgogoro kati “wavamizi” wanaoongozwa na Zitto na genge lake; na wenye chama chao, wanaoongozwa na Lucas Kadawi Limbu, mwenyekiti mwanzilishi wa ACT Tanzania.

Kama ndani ya ACT kuna demokrasia, ukilinganisha na huko walikotoka, Limbu na wenzake leo hii, wasingekuwa mahakamani kupinga kinachofanywa na Prof. Kitila na Mwigamba.

Kusingefanyika mapinduzi ya chama kwa kubadilisha katiba kinyemela; nembo ya chama, falsafa ya chama, kadi za chama, nembo ya chama na jina la chama.

Kama ndani ya ACT kungekuwa na demokrasia, kusingefanyika jitihada mahususi za kufukuza waasisi ili kumuandalia mtu mmoja; na mwenye maslahi binafi – Zitto Zuberi Kabwe – makazi ya kisiasa. Hata hicho cheo kipya cha kiongozi mkuu wa chama kisingeumbwa.

Kungekuwa na demokrasi, Anna Elias Mug’way, kwa jina jingine, Anna Shadrack Maghiya, angekuwa mwenyekiti halisi; na siyo kama alivyo sasa alikofanywa kama boya linaloelea baharini baada ya kukata nanga.

Yako wapi majukumu ya mwenyekiti ikiwa anayeitwa kiongozi mkuu wa chama, ndiye mkuu wa chama kwenye mikutano mikuu ya chama taifa, Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC)?

Yako wapi majukumu ya mwenyekiti ikiwa, kiongozi mkuu wa chama, ndiye atakayekuwa mkuu wa siasa, mshauri na mwelekezaji kwa viongozi wote na maafisa wa ACT-Tanzania?

Lakini kuna hili pia: Kama ndani ya ACT kungekuwa hakujengwi mtu; na kama ugomvi wa huko walikotoka ni kutokuwapo demokrasia, mbona hakuna utaratibu wa kugombea nafasi ya “Kiongozi Mkuu” wa chama?

Mbona mwenyekiti hana mamlaka ya kuagiza, kuteuwa; na au kuelekeza katibu mkuu wa chama ama mfanyakazi mtumishi mwingine wa chama? Madaraka yote yametupwa kwa kiongozi mkuu wa chama.

Iko wapi tofauti ya mfumo wa utawala wa kiongozi mkuu na utawala wa kifalme?

Katiba ambayo Zitto na wenzake wanatumia inasema, pamoja na mengine, kiongozi mkuu ndiye atateua wajumbe watano wa kamati kuu; ndiye mtoa tamko rasmi kuhusu masuala ya sera na mtazamo wa chama; mtoa habari mahususi kwenye mkutano mkuu, NEC na CC na masuala mengine ya kitaifa na kimataifa.

Kitila na wenzake wanaimba kuwa Zitto sasa ndiye atakuwa “nuru na taswira ya ACT-Tanzania ambayo wamegeuza jina na kuita ACT-Wazalendo.”

Katika mifumo ya kidemokrasia, “nuru na taswira” ya chama inakuwa mtu mmoja? Ni kitu gani hasa? Ni “zidumu fikra za Zitto?” Fikra zipi” Ni wanachama kumwacha Zitto awapeleka anakotaka? Ni ufalme wa Zitto?

Inawezekana kuwa hilo ndilo alikuwa anatafuta katika Chadema – na alikiri kuandaa – kupindua uongozi na watendaji ili achukue chama na kubaki dikiteta mkuu katika mfumo anaouita wa kidemorasia?

Yako wapi majigambo ya kupigania demokrasia? Kwa hili, hata wale ambao Zitto anatuhumu udikiteta, hawajawahi kujiundia uungu wa aina hii.

Nne, Zitto ameendela kudai kuwa katika miaka 10 ya ubunge wake, ameangusha serikali mara kadhaa. Akataja mkataba wa madini wa Buzwagi kwa kusema waziri wa nishati na madini alijiuzulu; na ukwapuaji katika sakata la Escrow.

Wote huu ni uongo mwingine mchafu. Hakuna waziri wa nishati na madini aliyejiuzulu kwa sababu ya kusaini mkataba wa madini wa Buzwagwi. Hakuna.

Aliyekuwa waziri wa wizara hiyo na aliyesaini mkataba wa Buzwagwi, Nazir Karamagi, alijiuzulu kutokana na kashifa ya Richmond iliyomg’oa waziri mkuu Edward Lowassa. Siyo Buzwagwi.

Kuhusu kashfa ya Escrow, kamati ya PAC iliyoongozwa na Zitto, haikufanya uchunguzi. Ilikabidhiwa ripoti ya uchunguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili iisome na kutoa maoni. Basi.

Kwenye sherehe ya kumuaga CAG, Ludovick Uttoh, mapema kabla ya mshikemshike wa Escrow kuanza, spika Anne Makinda alisema, baada ya kosoma ripoti, kuwa bunge lingekuwa linaendelea, “wengi” wangezama. Akamsifu Uttoh kwa kazi nzuri ya kuibua kashfa.

Sasa ambacho Zitto anajivunia kufanya katika kashfa ya Escrow ni kipi? Rekodi zipo. Kazi afanye CAG, sifa ajilundikie Zitto? Huu siyo uandilifu; lakini pia ni uongo wa kijinai.

Haya yameelezwa mara nyingi na yataendelea kuelezwa ili hatimaye, hata wale wachache waliosalia ambao hawajamfahamu vema Zitto, nao waweze kupata nuru.

error: Content is protected !!