September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

ACT ‘kuvunja mwiko’ Septemba 24

Spread the love

CHAMA cha ACT Wazalendo, kinajipanga kufanya mkutano mkubwa wa kidemokrasia utakaojumuisha viongozi, madiwani na wanachama wa chama hicho kwa lengo la kujadili mwenendo wa masuala mbalimbali hapa nchini, ikiwemo uchumi na siasa, anaandika Charles William.

Mkutano huo unatarajia kufanyika Jumamosi ya tarehe 24 Septemba mwaka huu, katika wakati ambao Rais John Magufuli pamoja na Jeshi la Polisi hapa nchini wamepiga marufuku mikutano ya hadhara ya kisiasa pamoja na ile ya ndani.

Hata hivyo Ado Shaibu, Katibu wa Kamati ya Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa ACT Wazalendo amesema, mkutano huo utafanyika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Katiba na taratibu za uendeshaji wa chama hicho na kwamba, hauhitaji kibali cha Jeshi la Polisi.

“Huu si Mkutano wa kuomba kibali polisi kabla ya kuufanya, ndiyo maana tunawakaribisha wananchi, wala sisi hatumjaribu Rais Magufuli kama alivyosema asijaribiwe bali sisi ni rafiki wa maendeleo,” amesema Ado.

Katika mkutano huo, chama hicho kinatarajia kujadili pia masuala mbalimbali yahusuyo bara la Afrika huku madiwani wote 42 wa chama hicho kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini wakitarajia kuhudhuria.

ACT inajipanga kufanya mkutano huo huku ikiwa na kumbukumbu ya kuzuiliwa kufanya baadhi ya mikutano yake ya ndani likiwemo kongamano lililoandaliwa na chama hicho kwa lengo kuchambua bajeti ya nchi katika ukumbi wa LAPF, Makumbusho Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ulipangwa kufanyika tarehe 12 Juni mwaka huu lakini ulizuiliwa na Jeshi la Polisi huku watu waliofika kuhudhuria wakizuiliwa kuingia ukumbini na jeshi hilo kutangaza kumsaka Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo ambaye baadaye alijisalimisha.

23 Juni mwaka huu, Rais Magufuli alitangaza kupiga marufuku mikutano ya kisiasa hapa nchini mpaka mwaka 2020 akidai kuwa, muda wa siasa umekwisha na kwamba wabunge na madiwani pekee ndiyo wataruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara katika kata na majimbo yao tu.

 

error: Content is protected !!