January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Abood aonesha jeuri ya fedha

Spread the love

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Abood Abdul-Aziz amesema, yupo tayari kumchangia fedha za kuweka mabango mgombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwenye jimbo hilo, Marcossy Albanie. Anaandika Charles William … (endelea).

Awali, Albanie alimtuhumu mgombea huyo wa CCM kwamba, anatuma vijana kubandua mabango yaliyobeba picha yake ikiwa ni sehemu ya kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.

Albanie ambaye anaungwa mkono na UKAWA alisema, pamona na Abood kutumia fedha na kuandaa vijana hao kuondoa mabango yake, pia amefanikiwa kudhibiti vyombo vya habari jimboni humo kutoripoti habari za mgombea huyo wa Chadema.

“Ninaendelea vizuri na kampeni zangu, changamoto kubwa ni nguvu ya fedha ya mpinzani wangu inayosababisha hata baadhi ya wanahabari kutoripoti taarifa zangu lakini pia mabango yangu yanachanwa kwa kasi,” alilalamika Albanie.

Hata hivyo, Abood amesema, “mimi mpaka sasa hivi kampeni sijaanza nipo Dar es Salaam. Sina wasiwasi kabisa na kampeni, kama mabango yake yanachanwa mwambie, Abood anasema nenda akuchangie uchapishe mengine. Aache kulialia,” Abood amesema.

Abood ambaye pia ni mbunge anayemaliza muda wake katika jimbo hilo amesema, madai ya mgombea mwenzake hayana msingi kwa kuwa yeye hahitaji mabango ili kushinda jimbo hilo.

“Wananchi wote wa Morogoro wananifahamu vyema kutokana na kazi kubwa niliyofanya kwa miaka mitano, sihitaji mabango ili kushinda kama yeye anayahitaji ili afahamike anitafute na nitamchangia au aniambie nimchapishie,” amesema.

Jimbo la Morogoro mjini lina jumla ya kata 29 huku vyama vinavyounda umoja wa UKAWA vikigawana kwa Chadema kusimamisha wagombea katika kata 19, CUF 9 na NCCR mageuzi 1 ili kukikabili CCM.

Kwenye jimbo hilo Abood pia anakabiliwa na Selemani Msindi (Afande Sele) wa Chama cha ACT Wazalendo.

error: Content is protected !!