Saturday , 13 April 2024
Habari za Siasa

Abdul Nondo atikisa

Mkurugenzi wa Idara ya Haki na Wajibu wa Wanafunzi Tanzania, Abdul Nondo
Spread the love

JESHI la polisi nchini, bado linaendelea kumshikilia, kinyume na sheria za nchi, Abdul Nondo, mwanafunzi wa mwaka wa tatu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kwa madai ya “kujiteka.” Anaripoti Saed Kubenea…(endelea).

Taarifa zinasema, Nondo anayeshikiliwa na jeshi hilo, tokea tarehe 7 Machi mwaka huu – siku zaidi ya 13 sasa – amenyimwa haki yake ya “kikatiba” ya kukutana na mawakili wake na ndugu zake.

Mwanafunzi huyo ambaye ni mwenyekiti wa mtandao wa wanafunzi wa vyuo vikuu (TSNP), alipotea katika mazingira ya kutatanisha, majira ya saa 5 hadi 6 usiku wa tarehe 6 Machi, huku baada ya kutuma ujumbe unaosema, “I AM AT HIGH RISK” (usalama wangu uko hatarini).

Mara baada ya Nondo kutuma ujumbe huo, taharuki kubwa iliibuka jijini Dar es Salaam kutokana na kutojulikana, nini hasa kilichomsibu kiongozi huyo wa wanafunzi.

Aidha, jeshi hilo halijaweza kumfikisha kumfikisha mahakamani kujibu kile polisi wanachoita, “tuhuma za kusingizia kujiteka.”

Kupatikana kwa taarifa kuwa Nondo amepotea, kulikuja takribani wiki mbili baada ya mauaji ya Akwilina Akwiline, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo cha usafirishaji cha taifa (NIT).

Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi “iliyorushwa na askari wa jeshi la polisi,” wakati jeshi hilo likidai kukabiliana na wafuasi Chadema, waliokuwa wanaelekea kwa msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kinondoni, kushinikiza kupewa hati za viapo kwa mawakala wake kusimamia uchaguzi.

Nondo, ni mmoja wa wanafunzi, ambaye amekuwa mstari wa mbele kushinikiza baadhi ya viongozi wa jeshi la polisi na wizara ya mambo ya ndani, akiwamo waziri wa wizara hiyo, Mwigullu Nchemba, kuwajibika kwa mauaji ya mwanafunzi huyo.

Nondo ayeripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha, alipatikana akiwa hai eneo la Mafinga mkoani Iringa. Alidai kuwa alijikuta katika eneo hilo, baada ya kuzinduka kutoka katika lindi la usingizi na kuwauliza wenyeji wa eneo hilo mahali aliko.

Baadaye alijisalimisha kituo cha polisi Mafinga, kabla ya kufikishwa makao makuu ya polisi mkoani humo kwa mahojiano.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kamanda wa polisi kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, amekiri jeshi lake kumshikilia Nondo.

Mambosasa amesema, Nondo hakuwa ametekwa, bali alikuwa akiendelea na shughuli zake za kawaida, kwa kumtembelea mpenzi wake.

Alisema, “taarifa kuwa Abdul Nondo aliyedaiwa kupotea katika mazingira ya kutekwa, ulikuwa ni uzushi kwani hakutekwa isipokuwa alikuwa kwa mpenzi wake.”

Hata hivyo, maelezo ya Mambosasa, yanatofautiana na ile ya jeshi la polisi mkoani Iringa, kuwa “Nondo alifika kituoni hapo akiwa hajitambui.”

Tayari mawakili wa Nondo wamewasilisha mahakama kuu maombi rasmi ya kutaka mwanafunzi huyo afikishwe mahakamani. Katika kesi hiyo, washitakiwa ni mkurugenzi wa mashitaka (DPP), mwanasheria mkuu wa serikali (AG) na mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP).

Nayo serikali ya Marekani, imetaka serikali ya Tanzania, kuingilia kati suala hilo na kusikitishwa na vitendo vya utekaji na ukatili nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Nchimbi aanika ugonjwa wa CCM

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emanuel Nchimbi,...

Habari za Siasa

Chadema yapuliza kipyenga uchaguzi viongozi kanda

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza maandalizi ya uchaguzi...

Habari za Siasa

CCM :Hatutaki ushindi wa makandokando uchaguzi Serikali za mitaa

Spread the loveCHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakihitaji ushindi wa makandokando katika...

Habari za Siasa

Makala: Puuzeni wanasiasa wanaojigamba wanaweza kubadili maamuzi ya mahakama

Spread the loveKATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),...

error: Content is protected !!