CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimemrudishia hadhi ya uanafunzi Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi (TSNP), Abdul Nondo baada ya kuondolewa chuoni hapo kutokana na kukabiliwa na kesi mahakamani. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa mitandao na Nondo, ameandika kuwa amepokea barua ya kurejeshwa chuoni hapo leo Ijumaa Januari 4, inayoeleza kuwa kuanzia tarehe 6 Januari, 2019 anaweza kuanza maandalizi ya kujiunga chuoni hapo kumalizi masomo yake.
Nondo alisimamishwa masomo yake baada ya kushitakiwa kwa makosa ya kudanganya kutekwa na kuchapisha taarifa za uongo mitandaoni iliyokuwa ikimkabili, kabla ya kushinda kesi hiyo tarehe 5 Novemba mwaka jana.
Mwenyekiti huyo aliandika katika walaka wao huo unaosambaa kuwa: “Barua hii imethibitisha mimi kurudishiwa sifa ya kuwa mwanafunzi wa UDSM kuanzia tarehe 6/1/2019 ambapo nitakuwa na haki ya kufanya maandalizi na kufuatilia taratibu zote za kujiandaa kuendelea na masomo semista ya pili kuanzia Machi 2019.
“Ikumbukwe mimi nilibakiza semista ya pili tu ya mwaka wa tatu ndiyo naanza kufuatilia taratibu za kumalizia semista hiyo hapo mwezi wa tatu baada ya mimi kupata barua hii ya kurejeshewa sifa yangu (status) ya uanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam. ni muda wa kujipanga kumalizia masomo yangu, hili ni jambo la msingi sana.”
Nondo amewashukuru uongozi wa UDSM kwa maamuzi ya busara waliochukua, lakini pia uongozi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na wananchi wote waliomsimamia kuanzia mwanzo mpaka mwisho wakati alipokuwa anapitia katika changamoto hizo.
Leave a comment