JUMLA ya watu sita wameripotiwa kupoteza maisha nchini Uganda na wengine 33 kujeruhiwa vibaya kutokana na milipuko ya bomu iliyotokea leo asubuhi tarehe 16 Novemba, 2021 katikati mwa jiji la Kampala nchini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea).
Polisi nchini humo wamesema milipuko hiyo miwili imetokea katika kituo cha ukaguzi cha polisi karibu na Kituo Kikuu cha polisi wakati mlipuko wa pili ukitokea karibu na geti la kuingia katika Bunge la nchi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini humo, Msemaji wa Polisi- Kamishna Fred Enanga amesema kwa mujibu wa kamera za CCTV, kati ya watu hao sita, watatu ndio waliokuwa wamebeba mabomu hayo na ndiyo waliojitoa mhanga na kufariki papo hapo.
Akizungumzia kuhusu majeruhi, Enanga amesema kati ya majeruhi hao 33, watano wako katika hali ya mahtuti na wengine 17 wamepelekwa katika hospitali mbalimbali nchini humo.
”Mlipuko wa kwanza ulitokea karibu na Kituo Kikuu cha Polisi jiji Kampala muda wa saa 10:03 asubuhi. Picha za kamera za CCTV zimeonesha mwanaume mmoja wa makamo aliyekuwa amevalia koti jeusi na begi mgongoni, alijilipua na kufariki papo hapo.
“Mlipuko huo umejeruhi polisi na raia wengine kutokana na waliokuwa umbali wa mita 30. Wengine wawili walithibitishwa kufariki wakati waliponea chupuchupu lakini wakiwa na majeraha mabaya,” amesema.
Aidha, amesema katika mlipuko wa pili ambao umetoka karibu na Bunge la nchi hiyo, umesabishwa na madareva bodaboda wawili waliojitoa mhanga.
Katika tukio hilo, raia mmoja amefariki papo hapo eneo ambalo pia lipo karibu na majengo makubwa ya Raj na Jubilee Insurance.
Amesema mshukiwa wanne, amekamatwa katika mtaa wa Bwaise jijini humo baada ya kupigwa risasi na polisi kisha kushindwa kujilipua kwa kujitoa mhanga.
Amesema mlipuko huo ambao umetokea ndani ya dakika tatu, saa 10:03 na 10: 06 asubuhi unahusishwa kikundi cha waasi cha Allied Democratic Forces (ADF).
Leave a comment