July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

815 waomba hifadhi nchini

Spread the love

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Kamati ya Kitaifa (NEC) imepokea maombi 815 ya raia wa nchi za nje wakihitaji hifadhi ya ukimbizi nchini, anaandika Regina Mkonde.

Isaac Nantanga, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi amesema maombi yao yanashughulikiwa ili kuona kama wanastahili kupewa hifadhi na kwamba, matokeo ya maombi yao yatatolewa hivi karibuni baada ya uchambuzi yakinifu kukamilika.

“Kati yao, 735 wametoka nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, 25 kutoka Burundi, 14 Rwanda, 15 Yemeni, 18 Syria, 3 Iran, 2 Kenya na 3 Eritrea,” amesema Nantanga.

Nantanga amesema kuwa, hadi kufikia tarehe 10 Februari mwaka 2016, wizara imepokea wakimbizi 129,210 kutoka nchini Burundi ambapo kati yao 79,290 wanahifadhiwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu mkoani Kigoma.

“Tangu Aprili mwaka jana nchi yetu imekuwa ikipokea wakimbizi wanaoingia nchini kuomba hifadhi kutokana na hali ya machafuko iliyotokea nchini mwao ambao wanahifadhiwa kwenye kambi za wakimbizi zilizoko mkoani Kigoma,” amesema na kuongeza;

“Wakimbizi 45,487 wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi Nduta iliyoko Kibondo na 4,543 wanahifadhiwa kambi ya Mtendeli iliyoko Wilaya ya Kakondo mkoani Kigoma.”

Nantanga amesema, wizara kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na wadau wengine, wametoa huduma muhimu za kijamii kwa wakimbizi hao.

“Wizara kwa kushirikiana na UNHCR na wadau wengine imekuwa ikitoa huduma muhimu kama vile za afya, chakula, maji na ulinzi ili kuhakikisha kuwa wakimbizi hawa wanaishi kwa usalama,” amesema.

Wizara ya Mambo ya Ndani imesema, Jeshi la Polisi, watumishi wa UNHCR na baadhi ya wakimbizi walioteuliwa na polisi, watashirikiana kufanya doria kwa wakimbizi wote ili kubaini wakimbizi watakao kuwa na nia ya kufanya uasi.

“Wakimbizi wanalindwa na Polisi ili kudhibiti baadhi ya wakimbizi watakaobainika kufanya maovu au kushirikiana na waasi kufanya maovu hasa kujaribu kuipindua Serikali yao,” amesema.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inaendelea na kampeni yake ya kuwakagua wageni wanaoishi nchini na kufanya kazi bila vibali vya kazi na ukaazi ili kuwachukulia hatua zinazostahili.

error: Content is protected !!