August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

8000 wajiandikisha kampeni kupinga ukatili wa kijinsia

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Dk. Dorothy Gwajima

Spread the love

 

JUMLA ya Watanzania 8000 wamejisajili kujiunga na kampeni ya Shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii (SMAUJATA) yenye lengo la kupinga na kupaza sauti kuhusu ukatili wa kijinsia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yameelezwa leo tarehe 30 Julai, 2022 na Waziri wa maendeleo ya Jamii, Dk. Doroth Gwajima wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu vipaumbele vya wizara hiyo kuelekea mwaka 2022/2023.

Amesema kampeni hiyo maalumu inayolenga kuhamasishaji wa jamii kushikiri kupinga ukatili wa kijinsia na watoto, imekuja na kauli mbiu isemayo ‘kataa ukatili wewe ni shujaa’.

Amesema kama alivyosema Rais Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya sikukuu ya mashujaa ni kwamba ushujaa sio kupigana vita pekee bali pia kupigania jambo lolote kwa maendeleo ya ustawi wa jamii.

“Tunahitaji mashujaa watakaopaza sauti bila uoga ili kuwa na kizazi chenye amani na furaha, ndio dhana ya kampeni imepata muitikio mkubwa ambapo watu 8000 wameshajiunga kutoka vijiji vyote… wanamsaka adui na kumkabidhi kwa vyombo vya sheria,” amesema.

Aidha, amesema wizara hiyo imekadiria kutumia kiasi cha Sh bilioni 43.4 ambazo pia zitatumika kuendesha ofisi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Pia ametaja vipaumbele nane vya wizara hiyo katika kuboresha huduma za maendeleo na ustawi wa jamii kuwa ni pamoja na kuratibu afua za kukuza usawa wa jinsia, uwezeshaji wanawake kiuchumi na kiuongozi na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, watoto na wazee.

Pili, kukuza ari ya jamii na kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi iliyoibuliwa ngazi ya jamii. Tatu, kutambua na kuratibu makundi maalumu wakiwamo wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga ili kubiresha mazingira ya biashara zao.

Nne, kuboresha mazingira ya kujifuanzia na kufundishia katika taasisi ya ustawi wa jamii, taasis ya maendeleo ya jamii Tengeru  na vyuo vya maendeleo ya jamii.

Tano, kuratibu utoaji wa huduma za msingi kwa watu wenye mahitaji maalumu, huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia na huduma msaada wa kisaikolojia kwa manusura wa  majanga mbalimbali na makundi mengine yenye uhitaji katika ndani ya jamii.

Sita, kuratibu na kuwezesha upatikanaji wa huduma za ustawi wa jamii wa wazee. Saba, kuratibu na kusimamia afua za upatikanaji wa haki za mtoto, ulinzi na malezi chanya ya watoto na mwisho ni kuimarisha ushiriki na mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa maendeleo ya Taifa.

error: Content is protected !!