JUMLA wanafunzi 800 wamehitimu masomo katika Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kati yao wanaume 279 sawa na asilimia 35 na wanawake 521 sawa na asilimia 65 katika Kampasi ya Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Akihutubia wahitimu hao wakati wa Mahafali ya 60 ya Taasisi hiyo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo tarehe Juni 30,2023 Mwenyekiti wa Baraza la Uendeshaji wa Taasisi hiyo, Dk. Naomi Katunzi amesema wahitimu wameweza kufuzu masomo kupitia programu mbalimbali zinazoendeshwa na TEWW, zikiwemo Elimu ya Watu Wazima na Mafunzo Endelezi, Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii pamoja na Elimu Masafa.

“Kwa upande wa programu za ngazi ya kati (Tertiary Level programmes) mnazoziendesha napenda kuwatia moyo kuendelea kutanua wigo wa utoaji wa mafunzo katika ngazi hii kwa njia ya masafa,” amesisitiza Dk. Katunzi.
Aidha, amesisitza kuwa ni muhimu kuhakikisha programu hizo zinaendeshwa kwa weledi na uzoefu kwa kuwa Taasisi hiyo ina wataalamu katika uendeshaji wa programu kwa njia ya masafa.
“Niwasihi kuendelea kutumia taaluma yenu katika kuboresha programu hizi kwa kuwa jamii bado ina uhitaji wa elimu. Sisi kama wana TEWW tuhakikishe tunaendelea kuhamasisha jamiii pamoja na wadau kwa kuzitangaza programu zetu ili kuweza kupata wateja wengi zaidi na hatimaye kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kutokuwa na fedha za kutosha,” amesisitiza Dk. Katunzi
Pia, Dk Katunzi ameipongeza TEWW kwa kuendelea kutekeleza malengo ya Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Kisomo na Elimu kwa Umma kwa kuendesha mafunzo kwa programu mbalimbali, ikiwemo programu ya MEMKWA, IPOSA na MUKEJA.
“Ni dhahiri maendeleo ya Taifa lolote hayawezi kufikiwa endapo watu wake si werevu. Ni imani yangu kupitia mpango Mkakati huu wa Kitaifa tutaendelea kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la kutojua KKK nchini kwa kuwafikia watu wengi zaidi wenye uhitaji wakiwemo vijana na watu wazima,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TEWW, Dk. Michael Ng’umbi amesema kwa kipindi kifupi cha mwaka huu Januari hadi Juni, 2023 jumla ya vituo 699 vilifunguliwa vyenye wanakisomo 3,502 nchi nzima.
“TEWW inatambua kuwa wanachuo ni jeshi kubwa ambalo likitumika vizuri litasaidia katika kufikia malengo ya Mkakati wa Kitaifa wa Kisomo na Elimu kwa Umma (NALMERS) wenye lengo la kuwafikia wanakisomo milioni mbili ifikapo 2025 na hivyo kuisaidia Serikali katika kupambana na adui ujinga”.amesisitiza Dk. Ngumbi
Kwa mwaka wa 2023/24 TEWW itaanza kutoa mafunzo katika kampasi mpya mbili za Ruvuma na Kilimanjaro na hivyo kuongeza udahili.
Vile vile TEWW itaanzisha mafunzo ya jioni kwa kampasi za Dar es Salaam na Morogoro. Pamoja na juhudi hizo, programu mpya zipatazo nane zinaandaliwa na zitakapokuwa tayari zitaanza kutolewa. Programu hizo zimejielekeza kwenye mafunzo ya amali na teknolojia, sawa na mwelekeo wa sera mpya ya elimu na mafunzo toleo la 2023.
Leave a comment