May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

800 wafariki dunia kwa UVIKO-19 Tanzania, wasiochanjwa hatarini

Spread the love

 

WATU 800 wamefariki dunia kati ya 33,726, waliothibitika kuwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) tangu kuripotiwa kwa kisa cha kwanza nchini hadi tarehe 4 Machi 2022. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamebainishwa jana tarehe 7 Machi 2022 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Aifello Sichalwe, wakati akitoa taarifa ya mwezi ya mwenendo wa UVIKO-19, kuanzia tarehe 5 Februari hadi 4 Machi 2022.

“Tokea ugonjwa huu ulivyoripotiwa kwa mara ya kwanza nchini mnamo Machi 2020 hadi kufikia tarehe 4 Machi 2022, jumla ya watu 33,726 wamethibitika kati ya 471,965 waliopimwa (7.1%) na watu 800 wamepoteza maisha (2.4%),” imesema taarifa ya Dk. Sichalwe.

Kuhusu mwenendo wa ugonjwa huo kwa mwezi, taarifa ya Dk. Sichalwe imesema kati ya tarehe 5 Februari hadi tarehe 4 Machi 2022, viliripotiwa visa vipya 290 vya waliothibitika kuwa na maambukizi ya UVIKO-19 , kati ya watu 31,090 waliopimwa ikiwa ni sawa na asilimia moja.

Taarifa hiyo imesema, Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa idadi kubwa ya waliothibitika ambayo ilikuwa ni watu 175.

Dk. Sichalwe kupitia taarifa hiyo amesema, asilimia kubwa ya wagonjwa walioathirika zaidi ni wale wasiochanjwa chanjo ya UVIKO-19.

“Wagonjwa wapya 136 walilazwa, kati ya hao 128 (94.1%) walikuwa hawajachanjwa. Kwa siku ya tarehe 4 Machi 2022, wagonjwa mahututi wanne waliripotiwa na wote walikuwa hawajachanjwa. Vifo nane vimeripotiwa kutoka Mikoa ya Mwanza (5), Dodoma (2) na Kagera (1) na wote walikuwa hawajachanjwa,” imesema taarifa ya Dk. Sichalwe.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Sichalwe amewashauri wananchi kupata dozi kamili ya chanjo ya UVIKO-19, sambamba na kuchukua hatua zote za kujikinga na ugonjwa huo, ikiwemo kuvaa barakoa wanapokuwa kwenye mikusanyiko, kunawa mikono mara kwa mara na maji tiririka, sabuni au kutumia vipukusi (Sanitizer).

“Serikali imeendelea kutoa chanjo kote nchini ili kuwezesha wananchi kupata kinga, mpaka kufikia tarehe 4 Machi 2022, jumla ya dozi 9,845,774 za chanjo ya UVIKO-19 zilikuwa zimepokelewa nchini. Tokea kuanza zoezi la uchanjaji jumla ya watu 2,664,373 wamepata dozi kamili ya chanjo,” imesema taarifa ya Dk. Sichalwe.

error: Content is protected !!