October 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Afisa kazi, kampuni ya Kascco akalia kuti kavu

Spread the love

RAIS Dk. John Magufuli, ametakiwa kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wa Idara ya kazi mkoa Mwanza, hususani Afisa Mkuu wa Idara ya Kazi, Khadija Hersia, kutokana na kushindwa kutatua migogoro mbalimbali ya wafanyakazi wa Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Kascco. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Afisa huyo na watumishi wa ofisi yake walalamikiwa na wafanyakazi zaidi ya 80 wa Kampuni ya uchimbaji wa madini Kascco, wanaoilalamikia ofisi hiyo kushindwa kutatua mgogoro uliopo baina yao na wamiliki wa kampuni hiyo ya kutokusainishwa mkataba wa kazi zaidi ya miaka 10 sasa.

Wafanyakazi hao wanaituhumu ofisi ya idara ya kazi kwa kushindwa kushughulikia madai yao na kusababisha wafanyakazi hao kuendelea kuteseka licha ya kuwepo chombo hicho cha serikali kinachoshughulikia matatizo ya wafanyakazi.

Wakizungumza na gazeti hili juzi wafanyakazi hao wanadai kwamba yapata mwezi mmoja sasa tangu waanze kwenda katika ofisi hiyo lakini mpaka sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Wamesema kuwa endapo kasi ya Rais Magufuli alionayo sasa, ataitumia kuwaondoa watumishi wazembe na mizigo kama waliopo katika ofisi hiyo ya Serikali, shughuli za kimaendeleo zitasonga mbele na kuondokana na watumishi wazembe serikalini.

Manyanyaso ya kampuni

Wafanyakazi hao wamedai kuwa wengi wa watumishi katika kampuni hiyo, wanafanya kazi bila mikataba zaidi ya miaka 10 sasa, lakini wanapotaka kudai haki yao hupewa vitisho kutoka kwa mwajiri wao, kitendo ambacho waliamua kukimbilia katika idara ya ajira.

Wanaeleza kuwa mara nyingi wafanyakazi wanapokuwa wakitaka kwenda katika idara husika uongozi wa kampuni hiyo hudai kwamba kokote kule watakapokwenda tayari wameishamalizana nao na kwamba hawatasaidiwa chochote.

Mmoja wa wafanyakazi hao, David Lembo anasema kuwa uongozi wa kampuni hiyo umekuwa ukidai kwamba tayari walishamalizana na viongozi wa idara ya kazi mkoa wa Mwanza pamoja na baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu ya mkoa huo.

Alidai kuwa uongozi wa kampuni hiyo umekuwa ukidai kwamba ni bora wasiwalipe wao mishahara na kuwapa mikataba ya kazi lakini watoe fedha kwa vigogo wa Serikali ili kuficha ukweli wa suala hilo kama wafanyakazi watakwenda kulalamika.

“Wafanyakazi wa Kascco (Kampuni ya Kascco) wanafanya kazi bila mikataba, wapo waliofanya miaka 10, saba, mitano na wengine mitatu, tunapojalibu kuomba mikataba ya kazi, viongozi huanza kutoa vitisho na wengine mpaka sasa tumefukuzwa.

“Mimi na mwenzangu, Gabriel Bahati, tumefukuzwa kazi kutokana na kuwa mstari wa mbele kudai haki yetu pamoja na ya wenzetu, sisi tumefanya kazi miaka 10 pale hatuna mikataba wala nini, tukiwaomba mikataba mgogoro unaanza, hali hii tumeichoka.

“Tunapo wauliza sababu zilizosababisha sisi kufukuzwa kazi kwamba ni baada ya wakaguzi na wanahabari kuenda kukagua kwenye kampuni hiyo kama wafanyakazi wana mikataba, ambapo walikuta wafanyakazi wote hawana mikataba,” amesema Lembo.

Hata hivyo anasema baada ya wakaguzi kuondoka kampuni hiyo ilianza kuaandaa mikataba, ambayo baada ya muda mfupi wafanyakazi waliitwa kusaini mikataba bila kuipitia, lakini yeye alipotaka kupewa muda wa kuipitia na kuupeleka kwa mwanasheria wake alikataliwa.

Pia anagusia kuwa kwa kipindi kirefu kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi yake kwa ujanja ujanja bila kuwasainisha wafanyakazi mikataba, kutokana na kubebwa na baadhi ya viongozi wa Serikali wasiokuwa waaminifu na wanaojali maslahi yao binafsi.

Amesema, “… wao wanasema tayari wameuweka uongozi wa idara ya kazi mfukoni pamoja na viongozi wakuu wa mkoa, kwamba walishamalizana nao, (anataja kiasi cha fedha kilichopokelewa na uongozi wa idara ya kazi ambacho kinahifadhiwa).

Pia aliwataja baadhi ya viongozi ambao uongozi wa kampuni hiyo, ambao umekuwa ukidai kumalizana nao ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo na Afisa wa Idara Kazi, Khadija Hersi ambaye anadaiwa kupokea Sh. 3 milioni.

Hata hivyo mfanyakazi huyo, alipohojiwa amefahamu vipi viongozi hao kupokea kiasi hicho cha fedha amesema, viongozi wa kampuni hiyo wamekuwa wakijitapa wao wenyewe, kwamba tayari walishawapa fedha, kwamba hata wakienda huko hawatasaidiwa.

Anasema kuwa sababu za ofisi ya idara ya kazi kushindwa kufuatilia suala lao ni kutokana tayari walishapokea kiasi hicho cha fedha, hivyo wanashindwa kufanya kazi yao kwa kufuata kanuni na sheria za utumishi wa umma.

Afisa wa Idara ya Kazi Mkoa wa Mwanza, Khadija Hersia, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alikiri kupokea malalamiko ya wafanyakazi hao kufukuzwa kazi na kuaahidi kuyashughulikia jumatano ya wiki ijayo.

Pia alidai kwamba tangu kampuni hiyo ianze kufanya kazi zake hajawahi kufanya ukaguzi wowote, pia hafahamu kama kuna wafanyakazi ambao hawana mikataba, hivyo suala hilo hawezi kulizungumzia zaidi.

Meneja wa Kampuni hiyo, Sairah Nuzrat, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo amesema kuwa mmoja wa wafanyakazi hao, David Lembo, alifukuzwa kwa sababu alimtukana, hivyo uongozi ukaamua kumfukuza kazi.

“Mimi kwanza sio msemaji wa kampuni, nitakupigia baadae uongee nae ambaye ndiye msemaji wa kampuni hii, hata hivyo baada ya muda mfupi mtu ambaye alitajwa ndiye msemaji wa kampuni hiyo, Jafesi Geresi, alikiri kuwepo madai hayo na kusema, “ …leo ni wikendi siwezi kuongea nitafute jumatatu,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia suala hilo, alisema kitendo cha kampuni lazima itachukuliwa kwani hakuna mtu aliye juu ya sheria.

error: Content is protected !!