Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Uingizaji holela vifaranga, chakula vyatesa wauza kuku
Habari Mchanganyiko

Uingizaji holela vifaranga, chakula vyatesa wauza kuku

Spread the love

UINGIZAJI holela vifaranga kutoka nje ya nchi na kupanda kwa bei ya chakula zimetajwa kukwamisha wazalishaji na wafugaji wa kuku wazawa, hivyo kusitisha biashara hiyo kwa madai kuwa wanapata hasara. Anaripoti Seleman Msuya…(endelea).

Aidha, wazalishaji na wafugaji wa kuku wameiomba Serikali kuweka mazingira ambayo yatawezesha wauzaji wa kuku kutumia mfumo wa kuuza kwa kilo kama wanavyouza wafanyabiasha wa nyama ya ng’ombe, mbuzi, kondoo na samaki.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kuzalisha Vifaranga ya Organia Albert Momdjian akielezea madhila wanayopitia kutokana na-soko la kuku kushuka nchini.

Hayo yamesemwa jana tarehe 3 Disemba, 2022 jijini Dar es Salaam na wazalishaji na wafugaji wa kuku wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto ambazo wanapitia kwenye sekta hiyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafuga Kuku (TABROFA), Costa Mrema amesema biashara ya kuku ina faida kubwa iwapo taratibu na sheria zitafutawa, hivyo kuiomba Serikali kuweka mkazo katika kuzuia  biashara ya vifaranga vinavyoletwa kutoka nje ya nchi kwa kuwa vimechangia kushuka kwa bei ya kuku sokoni na kuwapa hasara katika biashara hiyo.

Mrema amesema kuongezeka kwa kasi ya uingiaji wa vifaranga hivyo  umeporomosha soko la kuku kutoka Sh.5,500 hadi Sh.5,300, hali ambayo inaumiza wazalishaji na wafugaji wa ndani.

“Biashara ya kuku ina faida kubwa, imeajiri vijana wengi Wakitanzania, ila tunaomba Serikali idhibiti uingizaji wa kuku kutoka nje kwani inaharibu soko la ndani,” amesema.

Amesema kwa hali ya sasa Tanzania ni kama shamba la bibi katika sekta ya kuku ambapo kila mtu anaingiza vifaranga na asilimia kubwa havina ubora.

Aidha, Mwenyekiti huyo amesema wakati umefika kwa wafugaji wa kuku nchini kuuza kwa kilo kama ilivyo nyama ya ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Kwa upande wake Mshauri wa Sekta ya Kuku, Thabit Batenga amesema biashara ya vifaranga vya kuku inapitia wakati mgumu kutokana na kukosekana kwa ushindani halali.

“Tumeamua kukutana na wadau wa sekta hii, ili tuweze kujadiliana namna ya kukabiliana na changamoto hii ya kukosekana kwa ushindani halali, ili tupleleke serikalini kwa hatua zaidi,” amesema.

Naye, Mfugaji wa Kuku, Flora Kamote amesema uingizaji wa vifaranga na bei ya chakula kupanda, imesababisha yeye kuachana ufugaji kwa muda kwa kuwa mtaji wake unaisha.

“Mimi nafuga kuku kutoka Kampuni ya Organia, nimelazimika kuacha biashara hii kwa sasa, mfano mwezi wa 10 mwaka huu nimepata hasara baada ya kuuza kuku 2,000 Sh.5,000, huku gharama ya kukuza  kifaranga hadi unamuuza ikiwa ni Sh.6,300,” amesema.

Kamote ameiomba Serikali kuangalia changamoto hiyo kwa jicho la huruma kwa kuwa madhara yake ni vijana na wakina mama hasa wajane kukosa kazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi  Mtendaji wa Kampuni ya Kuzalisha Vifaranga ya Organia, Albert Momdjian  amesema vifaranga vinavyoletwa kutoka nje vinauzwa kwa bei ya Sh.1,000 na vinavyopatikana Tanzania vikiuzwa Sh.1,800, hali ambayo inaondoa dhana ya ushindani halali katika soko.

Momdjian amesema wameamua kukutana na wadau wa sekta hiyo, ili kujadiliana njia ya kutokana katika kadhia hiyo na kuishauri Serikali nini cha kufanya, ili kila upande upate haki.

Momdjian amesema uzalishaji vifaranga una gharama kubwa kama chakula, maji, umeme, dawa na mengine hivyo ikitokea kuna uingizaji wa vifaranga vya bei rahisi ni kuwaumiza wazalishaji na wafugaji wa ndani.

“Hali siyo nzuri katika biashara hii ya kuku, tunaomba Serikali iingilie janga hili, kwani wanaoumia sio sisi peke yetu bali na wateja wetu ndio maana tumeamua kusimama nao kwa kuwa bila wao sisi ni bure,”amesema.

Akizungumzia madai hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Hezron Nonga amesema Serikali ilitoa vibali vya kuingiza vifanga 2020/21 ila kwa mwaka huu haijatoa kibali chochote.

“Kampuni ya The One Agro Enterprises Ltd iliyoruhusiwa kuingiza vifaranga 494,000 na Wolowolo Animal Center vifaranga 150,000 na wote wameshaingiza, idadi iliyobaki hadi sasa ni vifaranga 364,000, wakimaliza hakuna kampuni nyingine itaruhusiwa,” amesema.

Aidha, amesema kushuka kwa bei ya kuku katika soko kunatokana na kipindi husika na hali ya uchumi na kwamba matarajio yao ni kuanzia sasa biashara itakuwa nzuri zaidi.

Mkurugenzi huyo amesema Serikali ipo macho kufuatilia watu wanaoingiza vifaranga kwa njia za panya, ili kulinda wazalishaji wa ndani.

Ametoa ushauri kwa kampuni za uzalishaji wa vifaranga kuzingatia ubora wa vifaranga ili kuwa na ushindani katika soko.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Gardner Habash wa Clouds Fm afariki dunia

Spread the loveALIYEKUWA mtangazaji wa kipindi cha Jahazi kinachorushwa na kituo cha...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

error: Content is protected !!