August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

70% ya Watanzania hawafanyi shughuli za kiuchumi

Spread the love

ASILIMIA 70.9 ya muda wa watu wenye umri kuanzia miaka 15 na kuendelea hutumika kwenye shughuli zisizo za uzalishaji ikilinganishwa na asilimia 18.5 inayotumika kwenye shughuli za kiuchumi…anaandika Aisha Amran.

Ofisi ya Taifa yaTakwimu (NBS), imesema takwimu hizo za matokeo ya utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2014 zitatumika kufanya maboresho ya mipango na sera mbalimbali za kukuza ajira na kupunguza umasikini nchini.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam Ruth Minja Kaimu Meneja wa Idara ya Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi hiyo amesema matokeo hayo yataiwezesha Serikali kuangalia upya tija ya utendaji kazi katika shughuli zinazofanywa na makundi mbalimbali ili kubaini mchango wake katika kukuza Pato la Taifa.

Amesema kwa mujibu wa utafiti huo Tanzania ina nguvu kazi ya Taifa ya watu 22.3 milioni wanaume wakiwa 11 milioni na wanawake wakiwa 11.2 milioni huku idadi ya watanzania walio nje ya nguvu kazi ya Taifa wakifikia milioni 3.4.

Amefafanua idadi ya watanzania walio kwenye ajira ni 20 milioni ikilinganishwa na watu 2.2 milioni ambao hawapo kwenye ajira.

Minja amebainisha kwamba kiwango cha nguvu kazi iliyo katika uzalishaji wa bidhaa na huduma za kiuchumi na nguvu kazi iliyo tayari kujihusisha na uzalishaji mali kimepungua kutoka asilimia 89.6 mwaka 2006 hadi asilimia 86.7 ya mwaka 2014.

Amesema kiwango cha watu wenye umri wa kufanya kazi walio na ajira kwa upande wa wanaume kwa mwaka 2006 kilifikia asilimia 80.8 ikilinganishwa na asilimia 82.1 za mwaka 2014 huku kiwango hicho hicho kwa upande wa wanawake kwa mwaka 2014 kikifikia 73.8 kutoka 77.6 za mwaka 2006.

“Kiwango cha watu wenye umri wa kufanya kazi walio na ajira kwa ujumla kimepungua, hii inaonesha kuwa, kiwango cha uchumi kuzalisha ajira kimepungua kidogo kutoka asilimia 79.2 mwaka 2006 hadi asilimia 77.8 mwaka 2014”Minja amesema.

Pia amebainisha masaa ya kufanya kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea kati ya mwaka 2006 hadi 2014 kumekuwa na ongezeko la masaa ambayo watu hufanya kazi kwa makundi yote ya ajira.

Aidha aliitaka serikali na wadau mbalimbali kushughulikia kiwango cha watu wasio na kazi na wale ambao hawako tayari kufanya kazi yoyote ya kiuchumi kutokana na ongezeko lake kuwa kubwa na athari kwa uchumi wa taifa.

error: Content is protected !!