ZAIDI ya watu 70 wanahofiwa kufa baada ya kuungua kwa ajali ya moto katika jengo la ghorofa tano ambalo linatumiwa na watu wasio na makazi katika mji wa biashara huko wilaya ya Kati, Johannesburg Afrika kusini. Anaripoti Isaya Temu, TUDARCo…(endelea).
Mapema leo muda wa saa 7:30 usiku siku ya Alhamisi tarehe 31 Agosti 2023 katika jengo la kibiashara la ghorofa 5 ulizuka moto mkubwa ambao chanzo chake hakijajulikana na kuunguza watu na mali zilizopo ndani ya jengo hilo.
Inaelezwa kuwa taktibani watu zaidi ya 70 mpaka sasa wanakisiwa kufikwa na umauti huku ikihofiwa kuwa idadi zaidi inaweza kuongezeka kwani uokozi unaendelea kwenye vyumba vingine vilivyoungua huku majeruhi wakiwa wanapatiwa matibabu ya haraka kabla ya kuwafikisha hospitalini.
Msemaji wa Huduma za Dharura Johannesburg, Robert Mulaudzi amesema kuwa watu wengine zaidi ya 40 wamepatikana wakiwa ni majeruhi huku akisema kuwa idadi ya majeruhi na vifo inaweza kuongezeka zaidi wakati uokozi ukiendelea.
“Zaidi ya miaka 20 yangu kuwepo katika huduma, sijawahi kukutana na kitu kama hiki,” Mulaudzi alisema.
Kupitia mtandao wa X, chama cha African National Congress(ANC), kimeeleza kusikitishwa na vifo vilivyotokana na moto huo.
“Tunahimiza mamlaka za kutekeleza sheria kuhakikisha kuwa wale waliohusika na janga hili wanawajibishwa,” ANC kimeandika kwenye chapisho kwenye mtandao X.
Mamlaka bado hazijabaini kwa usahihi chanzo cha moto huo lakini Mgcni Tshwaku, Afisa wa Serikali wa eneo hilo anaeleza kuwa ushahidi wa awali unahisi kuwa moto huo ulizuka kutoka kwenye mshumaa kwani wakazi wa jengo hilo hutumia mishumaa.
Adam Taiwo mmoja wa waathirika anaeleza ni kwa jinsi gani ameuepuka moto huo yeye pamoja na mtoto wake wa mwaka mmoja kwa kutoka nje ya ghorofa hilo kupitia dirishani.
“Kila kitu kilitokea kwa haraka sana na nilikuwa sina muda hivyo nilimwokoa mwanangu wa mwaka mmoja kwa kumtupa nje, nilimfuata pia kwa kupitia dirishani .” Taiwo alisema huku akiwa hajui sehemu ambayo mkewe Joyce yupo.
Takriban zaidi ya watu 200 walikuwa wakiishi katika jengo hilo, ikiwa ni pamoja na sehemu ya chini ya ardhi, ambayo ilipaswa kutumika kama karakana ya kuegesha magari. Huku mashuhuda Wengine wamekadiria idadi kubwa zaidi ya wakaaji.
Leave a comment