August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkakati CCBRT wapunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 47

Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi

Spread the love

 

MPANGO wa kuboresha huduma ya afya ya uzazi mkoa wa Dar es Salaam, inayoratibiwa na Hospitali ya CCBRT, imesaidia kupunguza vifo vya kina mama vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 47. Anaripoti Jonas Mushi, Dar es Salaam … (endelea)

Hayo yamebainishwa leo Jumanne tarehe 5 Julai, 2022 na Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi, wakati wa uzinduzi wa jengo la mama na mtoto katika hospitali hiyo.

Amesema CCBRT ilianzisha mpango wa kuboresha huduma za afya ya uzazi uliokuwa na awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilianza mwaka 2010 ikiwa na lengo la kuboresha huduma za afya katika vituo 27 vya umma.

“Mafanikio ya maboresho hayo ni pamoja na kupunguza vifo vya kina mama wanaojifungua kwa asilimia 47 na kupungua kwa viwango vya vifo vya watoto wachanga,” amesema Msangi.

Amesema CCBRT imeendelea kushirikiana na timu ya mkoa wa Dar es Salaam na halmashauri zake katika kuboresha huduma za afya ya uzazi na kwamba mafanikio hayo ni ishara ya ushrikiano huo.

Amesema awamu ya pili katika mpango huo ni ujenzi wa jengo jipya la mama na mtoto ambalo limezinduliwa leo.

Masangi amesema lengo kubwa la jengo hilo ni kuanzisha kitengo cha wazazi ili kuwahakikishia akina mama wote uzazi salama, kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi sambamba na kuzuia ulemavu.

Amesema kitengo hicho kimedhamiria kuhudumia akinamama wajawazito wenye ulemavu, wenye historia hatarishi ya uzazi, wenye historia ya fistula na mabinti waliopata mimba za utotoni.

Ameongeza kuwa jengo hilo limegharimu kiasi cha Sh101.2 bilioni ikijumuisha ujenzi, vifaa na vifaa tiba na usimamizi wa mradi.

error: Content is protected !!