January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kashililah naye ajitosa uspika

Spread the love

 

ALIYEWAHI kuwa Katibu wa Bunge la Tanzania, Dk. Thomas Kashililah ni miongoni mwa wanachama 66 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojitokeza kuchukua fomu kuwania kurithi nafasi iliyoachwa wazi na Job Ndugai ya uspika wa Bunge. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).

Hatua ya Dk. Kashililah kujitosa kwenye mbio hizo, kunazidisha fukuto la nani atakalia kiti hicho, katika uchaguzi utakaofanyika tarehe 1 Februari 2022, mkutano wa sita wa Bunge utakapoanza. Shughuli ya kwanza, itakuwa ni uchaguzi wa spika.

Hii ina maanisha, vigogo wa sasa wa Bunge kama Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu na waliowahi kuongoza Bunge kwa maana ya mwenyekiti, Andrew Chenge ambaye amewahi kuwa mwanasheria mkuu wa serikali watachuana kwenye kinyang’anyiro hicho.

Dk. Kashililah amechukua fomu leo Ijumaa, tarehe 14 Januari 2022, ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam akiwa kati ya wana-CCM 17 waliochukua leo Dar es Salaam, Dodoma pamoja na Zanzibar.

Mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu ulianza tarehe 10 Januari 2022 na utahitimishwa kesho Jumamosi, 15 Januari 2022.

Waliochukua fomu leo makao makuu Dodoma ni, Hatibu Mgeja, Dk. Linda Ole Saitabau na Mbunge wa zamani wa Makete, Profesa Norman Sigalla King.

Waliochukua fomu ofisi ndogo ya CCM Lumumba Dar es Salaam ni 12 ni, Emmanuel Sendama, Bibie Mssumi, Hilal Seif, Athumani Mfitakamba, Mwenda Mwenda na Mbunge wa zamani wa Ulanga, Goodluck Mlinga.

Wengine ni, Herry Kessy, Josephat Malima, Adam Mnyavanu, Andrew Kevela na Mbunge wa Nyasa, Stella Manyanya.

Waziri wa zamani wa mifugo na uvuvi ambaye sasa ni Mbunge wa Kisesa mkoani Mwanza, Luhaga Mpina yeye amechukua fomu yake Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar pamoja na Hussein Mataka.

Wote hao 66 na wengine watakaoongezeka, wanataka kurithi nafasi iliyoachwa wazi na Job Ndugai ambaye tarehe 6 Januari 2022, alitangaza kujizulu nafasi yake.

Alichukua uamuzi huo baada ya kauli aliyoitoa kuhusu serikali kuendelea kukopa kuibua mjadala mkali ndani ya chama chake huku akishinikizwa kujiuzulu naye akakubali.

error: Content is protected !!