September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Utata mtupu sakata la Meya Jacob

Boniface Jacob, aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo

Spread the love

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika amesema, chama chake, hakijawahi kumfukuza uwanachama, aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob. Anaripoti Hamis Mguta Salaam,Dar es Salaam…(endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili, tarehe 3 Mei 2020, makao makuu ya chama hicho, Ufipa jijini Dar es Salaam, Mnyika amesema, taarifa kuwa Jacob amevuliwa uwanachama, hazina ukweli wowote.

Boniface Jacob, Meya wa Manispaa ya Ubungo

Amesema, kutokana na hali hiyo, amemuandikia barua Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Betrice Dominick, kumtaka afute barua yake aliyomundikia Meya Jacob, kumtaarifu kuwa amepoteza sifa ya kuwa Meya wa manispaa hiyo.

“Chama kinamtambua Boniface kuwa ni mwanachama wa Chadema, Meya wa Manispaa ya Ubungo na ni diwani wa Kata ya Ubungo,” ameeleza Mnyika na kuongeza, “…nimemuandikia barua mkurugenzi wa manispaa ya Ubungo kumtaka afute barua yake aliyoandika jana na kuisambaza kwenye vyombo vya habari.”

Taarifa kuwa Jacob amepoteza sifa ya kuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, zilianza kusambaa kwa kasi kuanzia jana jioni, baada ya Betrice kunukuliwa na vyombo vya habari akisema, amepokea barua kutoka Chadema kata ya Ubungo, inayomjulishwa kuwa mwanasiasa huyo amevuliwa uwanachama na kata yake.

Kwa mujibu wa barua iliyotoka Chadema Kata ya Ubungo ambayo mkurugenzi huyo ameitumia kumuondoa Jacob kwenye kiti chake, imeeleza kuwa Kamati Tendaji ya Kata hiyo, katika kikao chake cha dharula cha tarehe 28 Aprili 2020, kilifikia maamuzi ya kumfukuza uwanachama, Ndugu Jaco, kutokana na kupatikana na hatia ya makosa kadhaa.

Miongoni mwa makosa ambayo yalitajwa, ni kutengeneza makundi chonganishi ndani ya chama; kusababisha migogoro na mitafaruku ya mara kwa mara.

Aidha, Jacob ametuhumiwa kuwatumia Betha Mwakasege, ambaye ametajwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), katika jimbo la Ubungo na mwanachama wa chama hicho, Rafii Juma (Macho), kuwakashifu baadhi ya viongozi wenzake ndani ya chama hicho.

“Tumechukua maamuzi haya, kwa kuwa tumechoshwa na migogoro yako ya mara kwa mara. Umekuwa bingwa wa kutengeneza makundi chonganishi, kinyume na Maelekezo ya Mwongozo wa Madiwani wa Chadema,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.

Inasema, “hivyo basi, Chama ngazi ya Kata, kimefikia maamuzi haya kwa kuzingatia Ibara ya 10.1 (ix) ya Katiba ya Chadema ya Mwaka 2006, Toleo la 2016, pamoja na vifungu 1 (b), (C) na (d) vya Kanuni za Chama.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo kwenye barua hiyo, kabla ya kufikia maamuzi hayo, uongozi wa kata yake unadai kuwa ulimuandikia barua ya kumjulisha kuwapo kwa kikao ambacho kilijadili uwanachama wake.

Lakini yeye kwa makusudi, hakufika kwenye kikao hicho na hakutoa taarifa wala hakuwasilisha utetezi wake.

Aidha, Chadema ya Kata ya Ubungo imeeleza kuwa wajumbe wa Kamati tendaji, kwa kauli moja, wamekubaliana kuwa ameshindwa kufanya kazi zake za udiwani, ikiwamo kuitisha mikutano ya hadhara na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chadema ya mwaka 2015, jambo ambalo “limesababisha Chadea kudhofika katika kata husika.”

Barua inayodaiwa kutoka Kata ya Ubungo na ambayo imesainiwa na katibu wa kata hiyo, Asheri Mlagwa, imebeba kichwa cha maneno kisemacho, “kufukuzwa uwachama,” ilikuwa na Kumb. Na. U/CDM/KUB/01/04.

Ilitumwa kwa Jacob na kunakiliwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo na Katibu wa Chadema wilaya ya Ubungo.

Akizungumzia utaratibu wa wachama wa Chadema kushughulikia matatizo ya meya wao, Mnyika alisema, Ibara ya 6 (3,6), Kifungu cha Saba cha Katiba ya chama hicho, kinaelekeza kuwa viongozi wa kitaifa, isipokuwa mwenyekiti na makamu mwenyekiti, mamlaka yao ya nidhamu, ni Kamati Kuu (CC) ya chama; Mstahiki Meya Jacob ni Mjumbe wa Kamati Kuu hivyo kwa nafasi yake, masuala yanayomuhusu hayawezi kushughulikiwa na ngazi ya Kata, wilaya wala Kanda.

“Tumemueleza Mkurugenzi vilevile hata kama mstahiki meya asingekuwa mjumbe wa kamati kuu kwa nafasi yake ya umeya utaratibu wa kinidhamu chama kina muongozo wa kusimamia, upo mwongozo wa kusimamia wabunge, halmashauri, madiwani na viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa na mameya.

“Katika kipengere cha 2 (i) kinasema kama kungekuwa na malalamiko juu ya utovu wa nidhamu au jambo lolote yanapaswa kufikishwa kwa Katibu Mkuu kwa maandishi ili yafikishwe kwenye kamati ya maadili ya taifa. Hivyo kwa nafasi hii masuala yake hayawezi kushughulikiwa na ngazi ya Kata, Wilaya wala Kanda, mimi kama Katibu Mkuu wa chama nilipaswa kupatiwa barua lakini sijapokea malalamiko yoyote kuhusiana na mstahiki meya,” ameeleza.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa kisiasa kwenye mitandao ya kijamii wanasema, hatua ya Mnyika kujitokeza kuzungumzia suala la mwanachama mmoja wa Chadema “kufukuzwa uwanachama,” inaonyesha ndani ya Chadema, hakuko sawa.

Amesema, “kuna watu wengi sana wamefukuzwa udiwani na viongozi wa wilaya, lakini Mnyika tangu akiwa Naibu Katibu Mkuu, hajawahi kuzungumzia suala hilo au kulikemea,” ameandika Anyabwile Mwaisile, ambaye alikuwa katibu wa Chadema, jimbo la Busekero.

“Ni Jambo la kawaida kabisa diwani kuvuliwa udiwani na Ngazi ya jimbo, wilaya na Kata. Mbeya hapa haya mambo yametokea mara nyingi sana. Mimi mwenyewe nimeitisha kikao na kumfukuza diwani wa kata ya Sisimba, alivuliwa na ngazi ya jimbo na sio Kamati Kuu kama Chadema wanavyotaka kutuaminisha.

“Naye diwani wa Kata ya Maanga, Newton Mwatujobe, alivuliwa uanachama na Ngazi ya jimbo sio Kamati Kuu kama Chadema Chadema wanavyotaka kutuaminisha; diwani wa Kata ya Iwambi, alivuliwa uanachama na jimbo na hata diwani wa Kata ya Nsalanga ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Meya wa jiji la mbeya alipewa onyo na jimbo baadae aliamua kuondoka kwa kujilinda ili asivuliwe uwanachama.”

Anaongeza: “Diwani wa Kata ya Kambasegela, Kiswigo Mwakalebela, alivuliwa uanachama na jimbo tofauti na Chadema wanavyotaka kutuaminisha. Lakini kubwa zaidi, Meya wa Jiji, Isaya Mwita, alivuliwa umeya na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinyemela kabisa, lakini siyo Mnyika wala viongozi wengine wa chama walihangaika na jambo hilo.

error: Content is protected !!