Spread the love

 

WANACHAMA 30 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamejitosa kumrithi Job Ndugai katika nafasi ya uspika wa Bunge la Tanzania. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Ndugai alijiuzulu uspika tarehe 6 Januari 2022, baada ya kauli yake aliyoitoa kuhusu serikali kuendelea kukopa fedha nje kuibua mjadala mkali ndani ya chama chake na kushinikizwa kujiuzulu.

Baada ya kujiuzulu, CCM ilitangaza kujaza nafasi hiyo kwa kuanza kutoa fomu za wanaohitaji nafasi hiyo kuanzia tarehe 10 hadi 15 Januari 2022, kisha mchakato mwingine wa kuwachuja utaendelea na hatimaye kupatikana mmoja.

Huyo mmoja atakwenda kushindanishwa na wa vyama vingine ikiwa watapeleka mgombea bungeni ambao watapigiwa kura na wabunge kisha mshindi atapatikana, tarehe 1 Februari 2022, siku mkutano wa sita wa Bunge utakapoanza.

Ikiwa leo Jumatano tarehe 12 Januari 2022, ni siku tatu tangu fomu zilipoanza kutolewa, wanachama na vigogo ndani ya chama hicho 30 wanachuana kuwania nafasi hiyo ya uongozi wa juu muhimili wa Bunge.

Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge

Solomon Itunda, Katibu msaidizi mkuu idara ya oganaizesheni wa CCM Taifa amesema, mpaka leo Jumatano Saa 10:00 jioni, wanachama 30 wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi ya uspika.

Fomu hizo zinatolewa Makao Makuu ‘White House’ jijini Dodoma, Ofisi Ndogo ya Lumumba, Dar es Salaam na Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar ambapo gharama yake ni Sh.1 milioni. Hivyo mpaka sasa CCM imejikusanyia Sh.30 milioni huku vigogo wakipishana kuchukua fomu.

Kati ya hao 30, wanawake ni wanne ambao ni Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, Asia Abdallah, Angelina John na waziri wa zamani katika serikali ya awamu ya nne aliyehudumu pia nafasi ya mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho Taifa (UWT), Sophia Simba.

Aidha, kuna Mwenyekiti wa Bunge ambaye ni Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu. Pia Zungu ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama.

Aidha wamo wabunge, Joseph Msukuma wa Geita Vijijini, Godwin Kunambi wa Mulimba mkoani Morogoro pamoja na Emmanuel Mwakasaka wa Tabora Mjini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Joseph Kasheku ‘Msukuma,’ Mbunge wa Geita Vijijini

Kuna mawaziri wa zamani wa mifugo na uvuvi, Dk. Titus Kamani ambaye mwaka 2015 alikuwa kati ya wanachama 38 wa CCM waliochukua na kurejesha fomu ya kuwania urais ndani ya chama hicho lakini hakufanikiwa.

Aliyewahi kuwa naibu waziri wa nishati na madini wakati wa utawala wa awamu ya nne wa Jakaya Kikwete akiwakilisha wananchi wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele naye amechukua fomu.

Masele amewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP).

Mbio hizo za kuwania uspika, zimemuibua aliyewahi kuwa mwanasheria mkuu wa serikali na mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge akiwania nafasi hiyo ya juu kabisa ya Bunge.

Katika hao 30, kuna msomi mwenye shahada mbalimbali tisa kutoka vyuo vya ndani na nje ya Tanzania, Profesa Handley Mafwenga aliyesema umefika wakati wa mtumishi kutoka serikalini kuongoza muhimili huo.

Wengine kwenye kinyang’anyiro hicho ni, Dk. Saimon Ngatunga, Tumsifu Mwansamale, Merkion Ndofu, Ambwene Kajula, Patrick Nkandi, Hamidu Chamani na Goodluck Ole-Madeve.

Pia, wamo Juma Chum, Baraka Byabato, Dk Musa Ngonyani, Faraji Rushagama, Hamisi Rajabu, Festo Kipate, George Nangale, Barua Mwakilanga, Zahoro Hanuna na Thomas Kirumbuyo.

Kutoka Zanzibar ambaye amechukua fomu ndani ya siku tatu ni mmoja, Mhandisi AbdulAziz Jaad Hussein.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *