April 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

24,528 waliomaliza kidato cha nne wameumizwa

Spread the love

JUMLA ya wanafunzi 24,528 sawa na asilimia 27.2 wenye sifa ya kujiunga na kidato cha tano pia vyuo vya ufundi wamekosa nafasi hiyo, anaandika Dany Tibason.

Wamekosa nafasi ya kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo Vikuu kutokana na ufinyu wa nafasi za shule za sekondari za kidato cha tano na vyuo hivyo.

Kauli hiyo imetolewa jana na George Simbachawene, Waziri wa Ofisi ya Rais, Taawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Ta,isemi), alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na vyuo vya ufundi kwa mwaka 2016.

Simbachawene amesema, kwa mwaka 2015 jumla ya wanafunzi 393,734 wakiwemo wasichana 200,919 na wavulana 192,815 walihitimu kidato cha nne.

Amesema, kati yao wanafunzi 90,380 wakiwemo wasichana 36,005 na wavulana 54,375 walifaulu daraja la kwanza hadi la tatu sawa na asilimia 22.95 ya wanafunzi wote.

“Wanafunzi hawa ndio walioshindanishwa kwenye uchaguzi wa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa mwaka 2016.

“Kati ya wanafunzi hawa 90,380 wanafunzi 90,248 wakiwemo wasichana 35,920 na wavulana 54,328 wanasifa za kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa mwaka 2016, sifa hizo ni pamoja na ufauru wa Credit tatu na usiopungua daraja la tatu la pointi 25” amesema Simbachawene.

Amesema, kulingana na utaratibu uliowekwa na serikali, mwanafunzi mwenye sifa za kuchaguliwa kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya ufundi ni yule aliyejaza fomu ya uchaguzi (Selform).

“Kwa kutumia fomu hiyo mwanafunzi ujaza machaguo matano ya tahasusi (Combinations)kwa masomo anayotaka kusoma na shule anayotarajia kujiunga nayo kwa kila chaguo” amesema.

Sinbachawene amesema jumla ya shule 326 zikiwemo shule mpya 47 zimepangiwa wanafunzi wa kidato cha tano kwa tahasusi mbalimbali.

Jumla ya wanafunzi 64,961 wakiwemo wasichana 28,911 na wavulana 36,050 sawa na asilimia 71.98 ya wanafunzi 90,248 waliostahili kuingia kidato cha tano kwaka 2016 wamechaguliwa.

Amesema kati ya wanafunzi waliochaguliwa 34,064 wakiwemo wasichana 13,466 na wavulana 20,598 watajiunga na masomo ya Sayansi na Hisabati  na wanafunzi 30,897 wakiwemo wasichana 15,445 na wavulana 15,452 sawa na asilimia 47.56 wamechaguliwa kusoma masomo ya Sanaa na Biashara.

Mbali na hayo Simbachawene amesema wanafunzi ambao wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi mwaka 2016 ni wanafunzi 759 wakiwemo wasichana 220 na wavulana 539 wamechaguliwa kujiunga na vyuo hivyo.

Kwa mujibu wa Simbachawene, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ina jukumu la Kusimamia,Kuratibu na kufuatilia shughuli Elimu ya awali,Msingi na sekondari.

“Kuanzia mwaka mwaka 2014 uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya Ufundi ni moja ya majukumu yanayosimamiwa na OR-TAMISEMI baada ya kugatuliwa madaraka kutoka Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia.

“Kwa mwaka 2016 zoezi la uchaguzi wa wanafunzi wa kuingi akidato cha tano katika shule za sekondari na vyuo vya Ufundi limefanyika na limekamilika”amesema Simbachawene.

Kutokana na hali hiyo Simbachawene,amesema wanafunzi wote wanatakiwa kuripoti katika shule walizopangwa kabla ya 25 Julai mwaka huu.

Amesema, endapo mwanafunzi atachelewa kuripoti, nafasi yake itachukuliwa na mwanafunzi mwingine aliyekosa nafasi.

 

error: Content is protected !!