Tume ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imethibitisha kupokea orodha ya wagombea 24 wa urais ambao wamejisajili kuwania katika uchaguzi wa Desemba 20. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa…(endelea).
Licha ya orodha hiyo, wagombea bado wanahitaji kuidhinishwa na mahakama ya kikatiba kabla ya orodha kamili ya wagombea kuchapishwa tarehe 18 ya mwezi Novemba.
Rais Felix Tshisekedi, aliyeingia madarakani mwaka wa 2018, amewasilisha ombi la lake la kuwania katika uchaguzi huo mapema Oktoba, akiwania kuongoza DRC kwa awamu ya pili.
Kutokana na kile ambacho kimetajwa kwa mgawanyiko katika muungano wa upinzani, Tshisekedi mwenye umri wa miaka 60, amepewa nafasi ya kuibuka mshindi kwa mujibu wa mtaalam wa masuala ya kisiasa nchini humo Christian Moleka.
Upinzani wa kisiasa ambao umetajwa kugawanyika utahitaji kumuunga mkono mgombea mmoja ili kupata nafasi ya kumshinda Tshisekedi, kulingana na Moleka.
Wapinzani wakubwa wa Tshisekedi ni pamoja na mshindi wa Tuzo ya Nobel, Dk. Denis Mukwege, mfanyabiashara tajiri na gavana wa zamani wa Katanga, Moise Katumbi na Martin Fayulu, mgombea ambaye hakufanikiwa mwaka wa 2018.
Mbunge Delly Sesanga na mawaziri wakuu wa zamani Adolphe Muzito na Augustin Matata Ponyo pia wako kwenye kinyang’anyiro hicho kwa awamu ya pili huku wakikabiliwa na mashtaka ya ubadhirifu.
Mwanamke mmoja pekee kati ya wagombea 24, Marie-Josee Ifoku Mputa, ambaye pia alishiriki katika uchaguzi wa 2018.
Hali ya kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa ya sintofahamu kwa miezi kadhaa, huku vyama vya upinzani vikidai kuwa uchaguzi huo hautakuwa wa wazi.
Uchaguzi wa urais unafanyika pamoja na uchaguzi wa wabunge, mikoa na manispaa, ambao maelfu ya wagombea wamejiandikisha.
Raia wa DRC wanatarajia kuwa kiongozi mpya atakayechaguliwa atasaidia nchi hiyo kukabiliana na changamoto za kiusalama katika eneo la mashariki.
Leave a comment