MAHAKAMA Kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam leo tarehe 10 Oktoba 2025, imeendelea na usikulizaji wa shauri Na. 19605/2025 la uhaini linalomkabili Tundu Lissu – Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambapo leo Lissu anamuuliza maswali ya dodoso (Cross Examination), shahidi wa pili wa serikali John Kaaya , ofisa wa Polisi anayefanya doria mtandaoni aliyehitimisha kutoa ushahidi wake jana tarehe 9 Oktoba saa 11 jioni.
Shauri hilo linalosikilizwa na jopo la majaji watatu wanaongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Jaji Dunstan Ndunguru, akishirikiana na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.
Kabla shauri hilo halijaanza Lissu alisimama na kuieleza mahakama hiyo kwamba wageni wake wamezuia na idara ya uhamiaji kuingia mahakama kwa kuwa hawana kibali.
“Lissu wale wageni wangu wameambiwa hawawezi kuingia ndani ya Mahakama hii hadi wapate kibali cha idara ya Uhamiaji Sasa wataendelea kuwepo hadi watakapofukuzwa kuwepo nchini hadi kibali chao cha kuwepo Tanzania kitakapoisha,” alidai Lissu.
Wakati huo huo Jaji Ndunguru, amesema kuwa mahakama hiyo ilishatoa utaratibu wa namna ya watu kuingia mahakamani hapo.
“Kwa hiyo tumeambiwa jambo hilo linashughulikiwa na ofisi ya msajili naomba ndugu zako wawasiliane na Ofisi ya Msajili ili wakalimalize,” amesema Jaji Ndunguru.
Baada ya kauli hiyo kesi inaendelea kusikilizwa na shahidi Kaaya yupo tayari kwa kujibu dodoso la lissu fuatilia kama ifuatavyo:-
Lissu: Inspekta John Kaaya ni majina yako?
Kaaya: Ndio.
Lissu: Nikikuuliza ndio au hapana jibu hivyo. Nikisema fafanua unafanya hivyo. Tukienda hivyo tutamaliza upesi. Usipofanya hivyo tutaenda mpaka week ijayo.
Lissu: Jana ulisema maneno yafuatayo ndio yalikufanya uone kauli yangu ya tarehe 3 Aprili yalikuwa na lengo la kuitisha Serikali “Tunahamasisha uasi, tutavuruga sana……” ulisema hivyo.
Kaaya: Ndio (akijibu kwa sauti ya chini sana).
Lissu: Ongeza sauti bwana we si ni askari.
Lissu: Uchaguzi upo kwa sheria ulisema. Ni kweli au sio kweli?
Kaaya: Anajibu kuwa ni Kweli.
Lissu: Ulisema kuzuia uchaguzi bila kufuata utaratibu kama vile kupata order ya mahakama nia yake ni kuitisha serikali?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Sasa eleza mahakama kwamba kwa miaka mingi zaidi ya miaka 30 viongozi na wanachama wamekuwa wakitumia njia ya mahakama kupinga mfumo huu wa Uchaguzi?
Kaaya: Hilo sifahamu.
Lissu: Unafahamu kama 1993 aliyekuwa Mwenyekiti wa Democratic Party Mtikila akipinga sheria za uchaguzi alifungua kesi mahakama kuu na kesi nyingine kupinga zuio la vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara?
Kaaya: Mimi sijui.
Lissu: Unanfahamu kama Mchungaji Mtikila vilevile alifungua mashauri hapa mahakama kuu kupinga zuio la watu wasio wa vyama vya siasa kugombea nafasi za kisiasa?
Kaaya: Nilikuwa Shule.
Lissu: We polisi nimekuuliza unafahamu au hufahamu?
Kaaya: Sijui.
Lissu: Jibu hivyo ili twende harakaharaka. Je kwenye kesi hiyo ya Mtikila mahakama kuu hii ilisema hicho kifungu cha Katiba kinachokataza watu kugombea wasio na vyama hakipo sahihi unafahamu hilo?
Kaaya: Mwaka gani ilikuwa?
Lissu: Mimi ndio nakuuliza Maswali au wewe? Haya unafahamu katika kesi ya Mtikila kupinga kifungu cha Katiba kinachozuia wagombea binafsi kilikubaliana na hoja zake na kifungu hicho kinakiuka misingi ya katiba na kifutwe?
Kaaya: Sifahamu.
Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu kwamba baada ya mahakama kuu kuamuru kifungu hicho kifutwe mahakama ya rufani ilitengua uamuzi huo na kusema kibaki?
Kaaya: Sifahamu kiukweli.
Lissu: Unafahamu kwamba baada ya mahakama ya rufani kumkatalia kukataa kufanya mabadiliko kwa njia mahakama alienda kufungua kesi mahakama ya Afrika kupinga mambo hayo?
Kaaya: Hilo Sifahamu.
Lissu: Waeleze unafahamu au hufahamu mwaka 2011 Mahakama ya Africa ya haki za binadamu iliiamuru Tanzania kufuta hivyo vifungu vinavyokataza wagombea huru?
Kaaya: Hilo sifahamu.
Lissu: Mwaka 2019 viongozi wafuatao Freeman Mbowe, Zitto Kabwe, Hasheem Spunda Rungwe, Seif Sharif Hamad na LHRC walifungua kesi mahakama ya Afrika Mashariki dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakipinga vifungu mbalimbali ya vyama vya siasa, Unafahamu hilo, Kama msajili kusema ondoa Mpina asiwe mgombea wa urais. Unafahamu hilo wewe polisi?
Kaaya: Hilo sifahamu.
Lissu: Tarehe 25 Machi 2022, mahakama hiyo iliitaka Tanzania kubadilisha hivyo vifungu?
Kaaya: Sikumbuki.
Lissu: Unafahamu Bob Chacha Wangwe, Mwanachama wa Chadema , alifungua kesi mwaka 2021 alifungua kesi akipinga Wakurugenzi kusimamia uchaguzi kwenye sheria za Tanzania? Unafahamu hilo?
Kaaya: Sikumbuki.
Lissu: Na unafahamu majaji walisema hivyo vifungu vinapaswa kufutwa?
Kaaya: Sikumbuki kabisa.
Lissu: Sasa waeleze majaji kama unakumbuka pia kwamba mahakama ya rufani ikasema uamuzi wa mahakama kuu haufai na ikautengua?
Kaaya: Sina kumbukumbu hizo.
Lissu: Kama unaelewa maana ya maneno yangu ya kwamba mahakamani hakuendeki? Maana mmesema kuwa nilisema kuwa mahakamani hakuendeki. Sasa sema maana ya niliposema mahakamani hakuendeki. Unaweza kuelewa maana ya hayo maneno?
Kaaya: Inategemea na maana anayoitaka.
Lissu: Naomba ajibu swali tafadhali waheshimiwa majaji. Swali langu ni rahisi.
Jaji: hebu jibu shahidi.
Kaaya: Naomba kueleza maudhui niliyosema mimi yapo kwenye video.
Jaji: shahidi hebu jibu swali ni rahisi.
Kaaya: Ndio nafahamu.
Jaji: Sasa sema yana maana gani?
Kaaya: Kauli ile ni constructive kwamba alianza kusema kuwa majaji ni watu wa Rais…
Lissu: Wewe polisi nimekuuliza maana ya maneno ya mahakama hakuendeki maana yake ni nini?
Kaaya: Majaji ni watu wa Rais na kwakuwa ni watu wa Rais basi ni MaCCM na majaji wanafanya kazi zao ili wapandishwe vyeo ili wapandishwe na kwenye tume ndio kuna hela.
Lissu: Hawa ndio wanaotulinda.
Lissu: Nikikueleza niliposema mahakama hakuendeki nilikuwa na maana kuwa tumeenda miaka 30 na mahakama zimetukatalia we unasemaje?
Kaaya: Sio kweli.
Lissu: Jibu kiafande mnatukoromea mitaani mkija hapa mnanywea.
Wakili wa Serikali Job Mrema analazimika kuingilia “mshitakiwa amepewa nafasi ya kuuliza maswali na kumuuliza kwa namna ya kumdhalilisha upande wa Jamhuri tunaona sio sawa”.
Lissu: Waheshimiwa majaji kila swali nimesema awaeleze majaji.
Jaji: Tuendelee hakuna kitu cha msingi hapo.
Lissu: Unajua nje ya mahakama kumekuwa na njia nyingine nje za kudai mabadiliko ya Katiba.
Kaaya: Sikuwepo kwenye jitihada hizo.
Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu kama mwezi Januari 1991 Rais Mwinyi aliunda tume ya Rais ya kama twende na chama kimoja au vingi?
Kaaya: Sina kumbukumbu hizo.
Lissu: Tarehe 17 Februali 1992 tume hiyo maarufu kama Tume ya Nyalali iliwasilisha taarifa yake kwa Rais Mwinyi?
Kaaya: Sifahamu.
Lissu: Mkiwa vituoni huko mnatukoromea sana, ongeza sauti na usiwe na wasiwasi kusema hufahamu Hautafungwa .
Lissu: Unafahamu kwamba Nyalali na tume yake walipendekeza kwamba nchi hii iwe na Katiba mpya itakapofika Septemba 1993?
Kaaya: Sijawahi kusikia kabisa hicho kitu.
Lissu: Unafahamu kwamba serikali ya Rais Mwinyi ilikataa mapendekezo ya tume ya Jaji Nyalali kuipatia Katiba Mpya?
Kaaya: Sina kumbukumbu.
Lissu: Umewahi kusoma kitabu cha Rais Mwinyi kunaitwa Mzee Rukhsa kinazungumzia historia yake?
Kaaya: Nimekisikia.
Lissu: Umekisoma Je?
Kaaya: Hapana sijasoma.
Lissu: Mzee Mwinyi kwenye kitabu hicho alieleza CCM na serikali walikataa mapendekezo ya Baba wa taifa kuwa mgombea binafsi aruhusiwe?
Kaaya: Sio kweli.
Lissu: Umejuaje wakati hujasoma?
Kaaya: Ni kweli sijasoma kwahiyo unaniuliza maswali ambayo sijasoma. Kwahiyo kiukweli sijasoma na sijui hayo mambo.
Lissu: Baada ya CCM kukataa mapendekezo ya Nyalali, Mkapa mwaka 1998 aliteua tume nyingine ya Jaji Kisanga ili kuangalia upya mfumo wa kikatiba.
Kaaya: Mimi sio mwanasiasa ndio maana siyajui hayo.
Lissu: Jaji Robert Kisanga alikuwa ni mwanasiasa?
Kaaya: Sifahamu.
Lissu: Sasa Unafahamu Jaji Kisanga aliteuliwa na Rais kuongoza tume hiyo mwaka 1998?
Kaaya: Huyo Jaji simfahamu na kazi zake sizifahamu.
Lissu: Mimi siwezi kukufunga ila napenda kukamata waongo kwahiyo hufahamu pia hata maamuzi ya tume yake?
Kaaya: Hayo yote sifahamu.
Lissu: Mwaka 2003 Rais Mkapa akaunda tume ya Jaji Mac Bomani kuongoza tume nyingine ya mabadiliko ya Katiba?
Kaaya: Sio sehemu yangu ya kazi.
Lissu: Unafahamu au hufahamu?
Kaaya: Sio sehemu ya kazi yangu kwahiyo sijui.
Lissu: Yalipokataliwa hujui pia?
Kaaya: Sijui kila kitu yani.
Lissu: Tarehe 31 desemba 2011, Jakaya Kikwete alitangaza ataunda tume ya Katiba ili ikusanye maoni ya Watanzania na kuandaa rasimu ya Katiba na itakapofika mwaka 2014 tuwe na Katiba Mpya?
Kaaya: Sijui.
Lissu: Unanfahamu Jaji Warioba aliteuliwa kuongoza tume hiyo?
Kaaya: Hilo nafahamu.
Lissu: Tume ya Warioba ilipendekeza kuwe na katiba mpya na kuandaa rasimu?
Kaaya: Hilo nafahamu lilikuwepo.
Lissu: Bunge maalumu la katiba lilikaa zaidi ya miezi 6?
Kaaya: Nafahamu na wewe ulikuwepo pia.
Lissu: Usiwe na kiherehere sasa. Nimeuliza unafahamu tu?
Lissu: Pamoja na kazi yote hiyo ya miaka minne CCM na serikali walikataa mapendekezo ya warioba na hakuna katiba mpaka leo?
Kaaya: Waheshimiwa majaji mchakato wa katiba ulianzishwa na serikali na bado upo kwenye utaratibu.
Lissu: Kwahiyo kuna utaratibu unaendelea toka 2013?
Kaaya: Mchakato unaendelea ulifika bungeni lakini taratibu zingine sifahamu kabisa.
Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu baada ya Kikwete kuondoka akaja Magufuli na baadae Samia. Mwaka 2022 Rais Samia walianzisha maridhiano mwaka huo?
Kaaya: Hayo nilisikia.
Lissu: Je unafahamu kama hayo mazungumzo yaliongozwa na watu wazito kama Kinana wa CCM na Freeman Mbowe kwa Chadema?
Kaaya: Sikushiriki.
Lissu: Unafahamu?
Kaaya: Sikushsiriki kwahiyo sifahamu
Lissu: Unajua Chadema ilipeleka mapendekezo ya namna ya kufufua mchakato wa katiba mpya ili hadi 2024 tuwe na katiba mpya?
Kaaya: Sikuwepo kwahiyo sifahamu.
Lissu: Je unafahamu tarehe 31 Mei 2023, CCM ilikataa mapendekezo yote ya Chadema na mazungumzo yale yakaishia hapo?
Kaaya: Nimeona kwenye vyombo vya habari kuna mambo yalifanyiwa kazi na serikali.
Lissu: Nimeuliza mapendekezo ya Chadema kuhusuu katiba mpya?
Kaaya: Sikushiriki kwahiyo sifahamu.
Lissu: Unafahamu kuwa desemba2021, Rais Samia aliunda kikosi kazi kuangalia matatizo ya mfumo wetu wa Uchaguzi na kumteua Prof. Rwekaza Mkandala kuangalia matatizo hayo?
Kaaya: Hilo nilisikia.
Lissu: Na mapendekezo ya kikosi kazi yalikataliwa na CCM na Samia huyu huyu?
Kaaya: Hilo nalo sifahamu.
Lissu: Sasa jitihada hizi toka mwaka 1991 hadi leo nikikwambia Chadema na mimi tumejaribu mahakamani imeshindikana na njia ya mazungumzo imeshindikana utasemaje?
Kaaya: Si kweli.
Lissu: Waeleze majaji tuna katiba mpya au hatuna? Fanya haraka jibu.
Kaaya: Tunatumia katiba ile ile ya zamani.
Lissu: Je uliwahi kuandika maelezo yako polisi?
Kaaya: Niliwahi kuandika.
Lissu: Je kama ukionyeshwa utayatambua?
Kaaya: Ni kweli nitayatambua.
Lissu: Waheshimiwa majaji sasa naomba nianze kumuonesha maeneo ninayotaka kuyalinganisha kulingana na ushahidi wake.
1. Eneo la kwanza alisoma chuo cha upolisi Zanzibar
2. Alipewa Cheti cha Competence.
3. Ushahidi wake juu ya masomo
aliyoyasoma kama vile kusomea masuala ya military and safety skills, sheria ya ushahidi.
5. Cheti alichopata baada ya training.
6. Alipelekwa kwenda kusomea nafasi ya assistant Inspector Moshi na kusomea community policing.
Lissu amemsomea takribani maeneo 40 ya maelezo yake.
Wakati huo huo wamakili wa serikali wanasimama na kupinga nyaraka ambazo Lissu anamsomea shahidi zisipokelewe kwa kuwa utaratibu wa kuwasilisha nyaraka hizo haujafuatwa .
Lissu: Waheshimiwa majaji wao wenyewe waliniletea hizi kesi siku ya kwanza leo nimetumia utaratibu huo huo ambao waliusema wao na kuniletea kesi tena wameona nongwa. “Kwahiyo naomba maelezo ya shahidi yapokelewe”.
Wakili wa Serikali Mwandamizi Igans Mwinuka akijibu hoja za Lissu amedai kuwa na kudai kuwa utaratibu aliotumia Lissu haukubaliki kisheria.
Wakati huo huo Jaji Ndunguru amesema kuwa wanahitaji muda wa kupitia hoja za pande zote mbili ili kutoa uamuzi na kuamua kuahirisha shauri hilo mpaka tarehe 13 Oktoba 2025,
Kesi hiyo itaendelea Jumatatu asubuhi saa 3:00 ambapo itakuwa ni tarehe 13 Oktoba 2025.
ZINAZOFANANA
Machafuko ya 29 Oktoba: Maaskofu Katoliki wataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wawajibike
Shinikizo la kufanyika uchunguzi wa mauaji ya 29 Oktoba lashika kasi
Meridianbet yaendelea kuwekeza kwa jamii kupitia MRC Rehabilitation Centre