Elibariki Kingu
MGOMBEA Ubunge wa Ikungi Magharibi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Elibariki Kingu, ameeleza kuwa Chama hicho kilikubaliana kwa pamoja kwa kuzingatia kanuni na taratibu kumpitisha Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea Urais wa Tanzania kupitia chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Singida … (endelea).
Akizungumza mbele ya Mgombea Urais huyo wakati wa Mkutano wa kampeni leo tarehe 9 Septemba 2025, Kingu ameahidi pia kumlinda na kumtetea Mgombea Urais huyo, na kuwataka watanzania kumpuuza mwanasiasa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole ambaye amekuwa akikosoa mchakato uliotumika kumpata Samia kuwania nafasi hiyo.
“Nikuambie Polepole, CCM tulikubaliana kwa pamoja, kwa kuzingatia kanuni na taratibu na tukampitisha Samia kuwa mgombea Urais, na Mwenyekiti wangu nikuhakikishie tutakulinda,” alisema Kingu.
Katika hatua nyingine Kingu amelitaja Jimbo la Ikungi kuwa na wapiga kura wengi wa CCM, akiwakosoa vikali wale wote wanaodai kuwa chama hicho na Mgombea Urais wake wamekuwa wakitumia nguvu kubwa katika kujaribu kupendwa na watanzania.
“Nikuambie mgombea wetu kuwa watu wote hawa wamekuja kwa mapenzi yao, kuna vikaragosi eti wanasema wewe unalazimisha kupendwa, naomba nikupe rekodi kuwa Jimbo la Ikungi Magharibi lina wapigakura 140,000, nataka nikuambie Oktoba 29, utazoa kura mpaka ushangae. Tembea kifua mbele, tutakulinda Dk. Samia,” smesema Mwanasiasa huyo.
Kingu pia amemshukuru Samia kwa utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo kwenye Jimbo la Ikungi Magharibi kwa miaka yake minne ya uongozi ikiwemo huduma ya maji, umeme, afya, elimu pamoja na ukuzaji wa diplomasia ya uchumi kote duniani, akiahidi kuzisaka kura za kishindo kwa Dk. Samia kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
ZINAZOFANANA
Mvutano wa kisheria wagubika Mahkama ya Z’bar
Hatuwezi kuongeza maslahi ya majaji kwa sasa – Samia
Rais Samia awateua Dk. Mpango na Majaliwa